0
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,  amewataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoingilia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kwa sababu hauwahusu.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho katika kikao cha ndani, kilichofanyika Wilaya ya Kinondoni ambapo alisema Chadema kushindwa kutekeleza Operesheni Ukuta ni dhahiri chama hicho kimeshindwa kutekeleza kile wanachoahidi kwa Watanzania.

Alisema mpaka sasa kumekua na vikao mbalimbali vinavyofanywa na viongozi wa Chadema kwa ajili ya kuivuruga CUF, jambo ambalo alisema haliwekezani.

“Chadema wanajitahidi kutuvuruga kwa kutuma waasi wa chama hiki, lakini naomba niwaambie hawawezi, CUF ni ngangari hata serikali inajua na  wanachokifanya ni kupoteza muda bure.

“Unajenga Ukuta wa biskuti, ukiumwagia juisi unamong’onyoka, Ukuta gani huo, huu muziki wa CUF ni ngangari hawauwezi,” alisema Lipumba.

Alisema katika kipindi hiki ambacho wana kesi mahakamani, wanachama wa chama hicho wataendelea na shughuli za kukijenga chama hicho pamoja na kuwasisitiza  kuwa na msimamo wa kutetea chama na katiba yake, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kufikia malengo waliyokusudia ya kushika dola kafika Uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema kutokana na hali hiyo, rasilimali za chama hicho zinasimamiwa kwa umakini chini ya walinzi wa chama hicho, Blue Guard ambao Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alisema ni wavamizi hawatambui.

“Ninamshangaa Maalim Seif sasa hivi anaibuka na kusema hawatambui walinzi wa chama Blue Guard ambao miaka yote walikua wanamlinda pamoja na rasilimali za chama, lakini hayo yamekwisha nitazidi kumwomba aje tujenge chama hata kama kesi inaendelea mahakamani,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano anayemunga mkono Profesa Lipumba, Abdallah Kambaya alisema kupoteza nafasi ya umeya na naibu wake katika Manispaa ya Kinondoni ni matokeo ya mgogoro wa CUF na kutokuwepo ushirikiano ndani ya Ukawa.

“Maalim Seif anaunga mkono Ukawa, mbona wanachama wa Ukawa wameshindwa kutusaidia ili kupata meya na naibu wake kwenye uchaguzi wa leo? (jana),” alihoji.

Post a Comment

 
Top