0

Serikali imefanikiwa kurejesha udhibiti wake kwenye Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) baada ya kurejeshewa asilimia 52 ya hisa zilizonunuliwa kinyume na utaratibu na Kampuni ya Simon Group Limited (SGL). 
 
Kurejeshwa kwa hisa hizo kunatokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba mauzo ya hisa hizo yaliyofanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa Uda hayakuwa na kibali cha Serikali. 
 
Ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15 ilibainisha licha ya utaratibu kukiukwa pia hakuna vilelezo vya fedha za manunuzi zaidi ya kuonyesha Sh320 milioni ziliingizwa kwenye akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Bodi, Idd Simba ambazo hata hivyo alidai ni malipo ya ushauri alioutoa kwa mwekezaji huo. 
 
Kurejeshwa kwa hisa hizo, kutolewa taarifa ndani ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo Jumanne ya wiki hii iliuweka kikaangoni uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusiana na sakata la Uda. 
 
Pia, kamati iliwataka Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) George Simbachawene, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju na Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru wafike kwenye kamati wakiwa na majibu sahihi kuhusu sakata hilo.
 
 Viongozi hao waliitikia wito huo jana, na baada ya kikao cha faragha Mwenyekiti wa LAAC , Vedasto Mwiru alisema Serikali imeitaarifu kamati yake kuwa imerejesha katika himaya yake fungu kuu la hisa ambazo hazikugawiwa. 
 
Mwiru alisema Serikali imerejesha hisa asilimia 52 ambazo ziliuzwa na Bodi ya Wakurugenzi Wa Uda kinyume cha utaratibu. 
 
“Maelezo yaliyotolewa na Serikali zile share (hisa) zote  ambazo hazikugawiwa ziko salama chini ya mikono  salama ya Serikali hazijauzwa,” alisema. 
 
Mwiru ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), alisema kutokana na maelezo hayo wabunge wametaka mikataba ya kurudisha hisa hizo kwa Serikali ipelekwe kwenye kamati hiyo. 
 
Alisema kamati hiyo inaipa Serikali muda wa wiki mbili kuhakikisha kuwa wanawasilisha nyaraka hizo. 
 
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema wanasubiri majibu ya barua yao ya kuomba ushauri kuhusu uuzwaji wa hisa za jiji za asilimia 51 kutoka kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Alisema baada ya kupokea ushauri huo watapeleka katika Baraza la Madiwani ili kuona namna ya kwenda mbele pamoja na kuzifanyia kazi fedha walizouza hisa zao ambazo ziko katika Benki Kuu (BoT). 
 
Mwanasheria Mkuu Masaju alisema anakwenda kuandika mambo yote yaliyosemwa ili iwasaidie kamati na Jiji la Dar es Salaam kukamilisha utaratibu huo kisheria.

Post a Comment

 
Top