Vigogo
watatu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) akiwemo
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Ephraim Mgawe (62)
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na rushwa ya Sh bilioni
nane.
Mbali
na Mgawe, vigogo wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa zamani wa
Uhandisi wa TPA, Bakari Kilo (59) na aliyekuwa Meneja wa Mazingira wa
TPA, Theophil Kimaro (54) pamoja na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni
ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).
Washtakiwa
hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka mawili na Wakili
wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba.
Wakili
Kishenyi alidai katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2009 na 2012,
Mgawe, Kilo na Kimaro kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ya Dola za
Marekani milioni nne ikiwa ni zaidi ya Sh bilioni nane.
Inadaiwa
waliomba rushwa hiyo kutoka kwa Shapriya ili kumuwezesha ashinde zabuni
iliyokuwa ikishindaniwa yenye namba AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili
ya ujenzi wa bomba la TPA katika RAS ya Mjimwema.
Aidha,
inadaiwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009 akiwa kama
Mkurugenzi wa DB Shapriya alitoa rushwa ya Dola za Marekani milioni nne
kwa vigogo hao, kwa ajili ya kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana kuhusika na kutenda
makosa hayo.
Wakili
Kishenyi alisema upelelezi wa kesi bado unaendelea, pia hawana
pingamizi la dhamana endapo washtakiwa watatimiza masharti ya dhamana
yatakayotolewa na mahakama.
Post a Comment