Siku chache baada ya Rais John Magufuli kusema kuna utoroshaji mkubwa
wa madini kupitia viwanja vya ndege vilivyopo migodini, Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) umekamata madini yenye thamani ya
Sh3,353,421,381.4 yakitoroshwa katika viwanja vikubwa vya ndege na
katika matukio 25 tofauti.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMAA, Mhandisi
Dominic Rwekaza ameeleza hayo katika ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na
wakala huo mwaka 2015 akisema: “Katika kufuatilia usafirishaji wa madini
nje ya nchi katika viwanja vikubwa tulikamata madini yanayotoroshwa
yenye thamani ya Dola za Marekani 1,512,186.61 na mengine ya
Sh34,670,794 katika matukio 25 tofauti.”
Akizungumza na wahariri wa
vyombo vya habari nchini hivi karibuni jijini, Rais Magufuli alisema
pamoja na kwamba Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini, kumekuwa na
utoroshwaji wa madini kwa ndege zinazoruka kutoka kwenye baadhi ya
migodi.
“Tuna dhahabu ambazo zinachimbwa, lakini utakuta watu
wanasafirisha makontena ya mchanga unapelekwa kwenda kusafishwa na sisi
ndiyo tunasindikiza na wananchi mpo mnashangilia,” alisema Rais
Magufuli.
“Kwa sababu kule wanakwenda ku-separate
(kutenganisha). Kwa nini tusijenge separation plant hapa tukatengeneza
ajira hapa kwa Watanzania,” alihoji.
Viwanja vya ndege migodini
Hata
hivyo, wakala huo umesema suala la migodi mikubwa kuwa na viwanja vya
ndege kwa ajili ya kusafirishia madini haliepukiki kwa sababu za
kiusalama.
Akifafanua ripoti ya ukaguzi wa madini ya mwaka 2015,
Msemaji wa TMAA, Isambe Shiwa alisema licha ya kudhibiti utoroshwaji
huo viwanja vya ndege vinatumika kusafirishia madini kutoka migodini
moja kwa moja kwa sababu za kiusalama.
“Katika maeneo yote ya
madini, kuna mawakala wa ukaguzi wa madini, wanashuhudia uzalishaji wa
madini, hasa kwa dhahabu wana chukua mikuo (mche wa dhahabu) yake na
kuileta kwenye maabara zetu ili ipimwe kujua kiasi cha dhahabu na fedha
kisha wanakokotoa mrabaha kulingana na madini husika,” alisema.
“Ili
kujua faida ya madini katika mgodi husika, huwa tunafanya ukaguzi
yakinifu na kukokotoa kodi zinazotakiwa hasa kodi ya shirika. Kama kuna
utata kwenye taarifa za mgodi kuhusu ununuzi wa vifaa na mitambo,
tunakagua na kuweka wazi gharama zake kisha tunapeleka TRA kiasi
kinachotakiwa kulipwa.”
“Kwa mfano ukiangalia bei ya madini ya dhahabu, kwa wastani gramu moja huuzwa Sh100,000, hivyo kilo moja huuzwa Sh1 bilioni.Ule
mkuo mmoja una kilo 20 hadi 25. Unaweza kuviweka vile vipande kwenye
mkoba ila ni vizito kubeba. Ukishazalisha hadi mikuo 20 ya dhahabu
unabeba mabilioni ya fedha, utasafirishaje kwa gari?
“Kuna
wakati pale mgodi wa Geita (GGM) kulikuwa na ndege iliyobeba dhahabu,
kumbe tayari watu walishatoa taarifa nje kwa watu waliojitayarisha na
silaha za kivita, wakaitungua ilipokuwa ikiruka. Bahati nzuri rubani
aliimudu na kufanikiwa kuirudisha uwanjani.”
Alisema kutokana na
matukio hayo, sasa wanasafirisha madini kwa helikopta ambayo ikichukua
mzigo hupaa kwenda juu zaidi kisha kwenda Dar es Salaam ambako
hukaguliwa tena kabla ya kwenda nje ya nchi.
“Kutokana na ukaguzi unaofanyika, naweza kusema hakuna madini wala mchanga unaosafirishwa kwa wizi kwenye migodi yote.Kwanza
hii migodi inamilikiwa na wana hisa walioko ndani na nje ya nchi. Wao
nao wanataka kupata taarifa za ukaguzi wetu ili wajue wanalipa kodi
kiasi gani na wanapata nini,” alisema.
Akizungumzia sababu za
madini ya tanzanite kuuzwa zaidi na Kenya, Afrika Kusini na India, Shiwa
alisema ni kutokana na Sheria ya Madini ambayo hukata mrabaha wa
asilimia tano ya madini hayo wakati sheria ya nchi hizo haina, hivyo
kuvutia zaidi wasafirisha madini kupitia nchi hiyo.
“Baada ya
kugundua udhaifu huo, kamishna wetu wa madini na ofisa mtendaji wetu
mkuu walikwenda Kenya kuzungumza nao ili nao waweke mrabaha huo na kweli
waliweka. Hivyo kwa miaka minne iliyopita madini hayo yamepungua sana
Kenya,” alisema.
Alisema wamechukua pia hatua ya kuongeza
thamani ya madini hayo kwa kuyakata baada ya kujenga viwanda mkoani
Arusha hivyo kupunguza usafirishaji wa madini ghafi kupitia Kenya,
Afrika Kusini na India.
Post a Comment