0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya China imetoa fursa ya kufungua soko la muhogo mkavu kutoka Tanzania, tukio ambalo  linafungua ukurasa mpya wa zao la muhogo kuwa miongoni mwa mazao ya biashara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake aliyoitoa wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge.

Amesema ili kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa hiyo, Mei 2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China. 

Amesema kufuatia hatua hiyo, mwezi huu wa Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo katika jimbo la Shandong.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kiasi cha muhogo kilichofanikiwa kuingizwa katika soko la China bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ambayo yanazidi tani 150,000 kwa mwaka.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha muhogo ambacho kimeonesha kuwa na tija kubwa, pia amevitaka vituo vya utafiti wa kilimo viwawezeshe wakulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa ili waongeze uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko hilo.

Waziri Mkuu amesema kutokana na zao la muhogo kuonekana kuwa na matumizi mengine zaidi ya chakula, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchakata muhogo na kuuzwa nchini China

Post a Comment

 
Top