0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 26,2018 amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI, hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Hii inakuwa ni kwa mara ya pili kwa Waziri Mkuu Majaliwa kumtembelea kumjulia hali ambapo awali alimtembelea Jumapili ya Agosti 5, 2018), wakati Dkt. Kigwangalla akipatiwa matibabu ya awali katika Wodi ya Mwaisela. Akiwa wodini hapo, Waziri Mkuu Majaliwa amemtakia kila lakheri katika kuuguza mkono wake ambapo pia amepata kuzungumza nae juu ya maendeleo ya afya yake.

Aidha, Waziri Majaliwa amewashukuru Madaktari wa MOI pamoja na uongozi wake kwa pamoja kutoa huduma bora kwa watanzania na raia wa Nchi za nje ambao wamekuwa kimbilio kuja nchini kupata tiba.

“Nakutakia kila lakheri Kigwangalla. Nimekuja baada ya kusikia umefanyiwa operesheni ya pili. Pia nawashukuru Uongozi na Madaktari wetu wa hapa MOI kwa kutoa tiba nzuri tiba zenu kwa sasa zimezifanya nchi zingine wananchi wake kukimbilia hapa. Viongozi wakuu pia Hospitali hii ndio kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru kwa huduma bora inayofanya Nchi kuwa na heshima kuwbwa,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande wake Dkt. Kigwangalla amemwakikishia Waziri Mkuu kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kwani ameweza kufanya mazoezi ya ikiwemo kutembea umbali wa kilometa nne pamoja na mazoezi mepesi kila siku majira ya asubuhi na jioni.

“Kwa sasa naendelea vizuri sehemu kubwa ni mkono ndio nauguza. Ila kwa hali ya maendeleo kwa sasa naendelea vizuri pamoja na mazoezi kidogo kidogo naendelea. Alisema Kigwangalla. Aidha, mbali na Waziri Mkuu Majaliwa, jana jioni Agosti 25,2018, Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliweza kumtembelea tena na kumjulia hali.

Dkt. Kigwangalla alipata ajali asubuhi ya Jumamosi, Agosti 4, 2018) katikati ya vijiji vya Mdolii na Minjingu wilaya ya Babati mkoani Manyara baada ya gari lake kupinduka na kusababisha kifo cha Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Hamza Temba na wengine watano akiwemo Dkt. Kigwangalla kujeruhiwa.

Post a Comment

 
Top