0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 07 Oktoba, 2016 amekutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na mambo mengine ametaka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Katika Mkutano huo uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Rais Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya shughuli za mabalozi, alisema Tanzania imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.

“Sasa nimeona niwaite waheshimiwa Mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda.

“Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu” alisema Rais Magufuli.

Maeneo mengine ambayo Rais Magufuli ametaka Mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na kuwavutia watalii kuja hapa nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanakowakilisha.

Pia Rais Magufuli aliwataka waheshimiwa Mabalozi wote kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.

Dkt. Magufuli aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima, pamoja na kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi kwenye nchi mbalimbali bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa Serikali.

“Kuna wafanyakazi wapo kwenye Balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika nafasi wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa ubalozini.

“Wakati mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani” alisisitiza Rais Magufuli.

Hata hivyo Dkt. Magufuli aliwapongeza Mabalozi wote wa Tanzania kwa kazi wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na amewahakikishia kuwa Serikali ina matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha na kuitangaza vizuri Tanzania.

Mkutano huo pia ulihuduriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa Taasisi mbalimbali na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

Post a Comment

 
Top