Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka
serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi
katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.
Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).
Alisema
hayo jana mjini Dodoma wakati akikabidhi taarifa ya tathimini baada ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
Tathimini
hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk
John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Lubuva
alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya
343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu
vinavyokinzana.
“Pamoja
na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini
na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa uhuru
zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi wa
halmashauri,” alisema.
Alisema
baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini
kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka
kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1993.
“Tathimini
hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha mzunguko wa
uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,” alisema.
Alisema
changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na
mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile
alilojiandikisha.
Pia
wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa
mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha
na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.
Alisema
tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga
kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha
kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Baadhi
ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa
kupiga kura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura wengi,
pia wapigakura walijiandikisha katika daftari la kudumu kwa ajili ya
matumizi mengine ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo
wa hofu, vitisho na vurugu siku ya kupigakura,” alisema.
Waziri Mhagama, Mkurugenzi wanena
Kwa
upande wake, Waziri Mhagama alisema tume inapaswa kupongezwa kwa
kukamilisha zoezi zima la Uchaguzi Mkuu, ambalo lilikuwa na changamoto
nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa.
Alisema
kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura
343, tume inapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili
kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine, lakini haikuwezekana kufanyika
hivyo baina ya mwaka 2010 na mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.
Alisema
sababu hizo ni pamoja na ufinyu wa bajeti na kuchelewa kupatikana kwa
fedha kwa wakati, lakini serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa mapungufu
yaliyo ndani ya uwezo wake, yanatatuliwa ili kuiwezesha tume kutekeleza
majukumu yake ya kikatiba na kisheria kwa wakati.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015 ilifanyika, ikiwa ni hatua ya kukamilisha mzunguko wa
uchaguzi.
Alisema
kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa, watendaji 929 ambao ni sawa na
asilimia 90.3 walisema wana uelewa kuhusu muundo wa tume na watendaji
100 sawa na asilimia 9.7, walikuwa hawana uelewa kuhusu muundo wa tume.
“Kati
ya watendaji 929 wa uchaguzi waliohojiwa, 818 sawa na asilimia 88
walisema kuwa muundo wa tume unafaa kuendesha uchaguzi, aidha watendaji
111 sawa na asilimia 12 walieleza kuwa muundo wa tume haufai katika
kuendesha uchaguzi,” alisema.
Pia
matokeo yanaonesha kuwa, katika watendaji wa uchaguzi 1,014
waliohojiwa, 814 sawa na asilimia 80.3 walisema hakukuwa na changamoto
katika njia hizo, watendaji 200 sawa na asilimia 19.7 walieleza njia za
mawasiliano zilikuwa na changamoto.
Alisema
matokeo ya tathimini yameonesha kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa 996
sawa na asilimia 96.8 walikuwa na maoni kuwa utekelezaji wa majukumu ya
uchaguzi ulizingatia maelekezo yaliyotolewa na tume, ambapo watendaji
33 sawa na asilimia 3.2 walieleza kuwa utekelezaji haukuzingatia
maelekezo hayo.
Aidha
alisema wadau wa uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu uelewa wao juu ya
elimu ya mpiga kura, kati ya wadau 1,463 sawa na asilimia 76.4 walisema
walikuwa na uelewa wa elimu ya mpiga kura na 452 sawa na asilimia 23.6
hawakuwa na uelewa.
Kailima
alisema wapiga kura 499 walihojiwa, ambapo kati yao wapiga kura 377
sawa na asilimia 75.6 walisema walitumia chini ya dakika 30 kufika kituo
cha kupiga kura, wakati wapiga kura 87 sawa na asilimia 17.5 walitumia
dakika 30 hadi 60 kufika kituo cha kupiga kura.
Post a Comment