0
Wakati taariza zinazomtuhumu Profesa Ibrahim Lipumba kufungua akaunti benki kwa lengo la kuingiziwa fedha za ruzuku ya Chama cha Wananchi (CUF) kinyume cha sheria kwa ajili ya kukivuruga chama hicho zikienea.

Bodi ya Wadhamini ya CUF imetoa onyo pamoja na kuwatahadharisha watu wanaotumika kusaini nyaraka feki kwa lengo la kufungua akaunti hizo, pia imezitahadharisha benki zote nchini kutofungua akaunti yoyote kwa jina la CUF pasipo kupata muhtasari wa bodi halali ya chama hicho.

Katika hatua nyengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro amefafanua kuwa wenye mamkaka halali ya kufungua akaunti ya chama hicho ni Bodi yake ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi.

“Tunatoa onyo, kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwamba tumeshafungua shauri na utaratibu wa kisheria umeshaanza kuchukua mkondo wake, tumesikitika kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kinyume cha sheria namba tano 1992 ya vyama vya siasa na kinyume cha katiba, Msajili kwa mara ya kwanza anaziandikia benki zilizosajiliwa na BOT akizitaka kumfungulia akaunti Lipumba za kuwekea fedha,” amesema Mtatiro.

Mtatiro amedai kuwa ”Benki itakayomfungulia akaunti Lipumba ni makosa makubwa. Sababu huwezi fungua akaunti ya taasisi au chama bila ya bodi yake ya wadhamini kukaa kikao na kuandaa muhtasari kwa ajili ya kupeleka benki ili kufungua akaunti.Lipumba na watu wake wameandaa nyaraka feki pamoja na barua ya msajili kutaka kufungua akaunti. Tunajua amepeleka katika benki mbalimbali,

“NMB ilikataa sasa wanapeleka benki ya Exim na ilishapewa taarifa kuwa uhuni huu haukubaliki na masuala ya fedha yako chini ya katibu mkuu kwa mujibu wa katiba ya cuf,” amesema.

Sambamba na onyo lililotolewa na bodi hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam leo imekubali maombi yake ya kufungua shauri la kuitaka mahakama hiyo kutoa amri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi ya kutoendesha shughuli zake za usimamizi wa vyama vya siasa kinyume cha sheria, pamoja na kutengua barua yake inayomtambua profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili Juma Nassoro amesema kuwa Jaji wa mahakama hiyo Munisi, amekubali maombi yao na kwamba jopo la mawakili wa CUF linatarajia kuwasilisha maombi rasmi wiki hii.

“Jaji Munisi baada ya kutusikiliza vifungu vya sheria tulivyotumia, Mahakama imekubali ombi letu ili tuweze kufungua maombi ya kuomba mahakama itamke kufuta barua ya msajili inayomtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF. Pia Itoe zuio rasmi kwa msajili kutofanya shughuli zake nje ya utaratibu ambao amepewa chini ya sheria ya vyama vya siasa,” amesema Nassoro.

Amesema baada ya mahakama kuridhia maombi yao, iliwataka kuwasilisha maombi rasmi ndani ya siku14 kuanzia leo.

“Tumeambiwa tuwasilishe maombi ndani ya siku 14, lakini tutayawasilisha ndani ya siku Saba na tutaiomba mahakakama iyasikilize kwa Hati ya dharula ili shughuli za chama ziendelee,” amesema.

Post a Comment

 
Top