Mbunge wa Budalang’i nchini Kenya, Ababu Namwamba amesema Rais John Magufuli anavuma kwa umashuhuri nchini humo akitajwa kwa namna anavyopambana na ufisadi na kubana matumizi ya Serikali, lakini akasema sifa hizo zitapendeza iwapo huduma muhimu kwa wananchi zitaboreshwa na kuthibitika kwenye tafiti zitakazofanywa.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati alipohudhuria mkutano wa demokrasia
ulioandaliwa na ACT – Wazalendo jana, Namwamba ambaye pia ni kiongozi wa
chama cha Labour of Kenya (LPK), alisema Rais Magufuli ana mtandao
Kenya unaomshabikia kwa uongozi wake, ikiwamo harakati zake za kupambana
na ufisadi
“Lakini
swali kuu katika fikra za Wakenya wengi ni sasa je, mambo yote
tunayoona kwenye vyombo vya habari ni porojo tu ama ile inaitwa
propaganda au ni masuala kweli yanayobadili maisha ya Watanzania wengi?
Hivyo ingawa sifa za Magufuli zinaenea huku na kule, tungependa kuona
mabadiliko halisi hapa Tanzania,” alisema.
“Tungependa
kuona kwa mfano takwimu za ufisadi zimepungua. Takwimu za kuonyesha
hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida imebadilika huduma kama vile
maji, elimu na afya kwamba kweli zimebadilika hilo ndilo la muhimu
zaidi, kinyume cha hapo hatutapata sababu ya kuamini au kuona kwamba
mabadiliko hayo ni halisi.”
Namwamba,
ambaye Julai 7 mwaka huu alijiuzulu ukatibu mkuu wa chama cha ODM
kinachoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Raila Odinga baada ya
kutoelewana, alisema siasa za nchi hizo mbili zinakaribiana kwa kuwa
mashindano ya wanasiasa yaliyopo nchini ni kama yalivyo Kenya.
“Kila mara mnapokuwa na uchaguzi hapa sisi hutazama kwa makini sana kwa sababu kuna mengi ya kujifunza.
"
Hata
hivyo, Namwamba alionya kuwa suala la ukabila nchini ni la kutiliwa
maanani kwa kuwa kufanya siasa kwa misingi hiyo kumesababisha maafa
makubwa ikiwamo mgawanyiko kwa wananchi.
Alisema
siasa nzuri zinazopaswa kuendelezwa nchini ni zile za kuwaleta wananchi
pamoja na kama ni mashindano, yawe ya sera, dhana, huduma bora kuliko
kumtazama kiongozi wa chama au mgombea kwa kabila lake.
Alisema
amekuja nchini kushirikiana na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe
kupanda mbegu ya ushirikiano na kwamba atashiriki kuhamasisha vijana
kutambua viongozi walioweka historia wakiwamo Mwalimu Julius Nyerere na
Nelson Mandela.
Zitto
akizungumza katika mkutano huo alieleza kuwa chama chake kinaunga mkono
juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kurejesha nidhamu ya kazi
kwa watumishi wa umma na kupambana na ufisadi.
“Lakini
tungependa kuona hatua zinachukuliwa zaidi ikiwa ni pamoja na
kuwafikisha kwenye vyombo vinavyohusika watumishi 154 wachukuliwe hatua
zinazostahili.Pia suala la Escrow nalo linapaswa kuchukuliwa hatua na
mengine mengi.”
Mshauri
wa ACT, Profesa Kitila Mkumbo aliwasilisha mada ya; “Sisi ni kina
nani?” akilenga kuwaelimisha wanachama wake kujihusisha na maisha ya
watu, kwa kuwa kushughulikia changamoto na matatizo ni mchakato
unaoendelea iwe ndani au nje ya Serikali.
“Chama
chetu siyo cha kuvizia makosa ya Serikali ndipo tufanye siasa,
tunajipanga kushindanisha ubora wa sera, kina itikadi yake kamili, ni
jukumu letu kukosoa Serikali lakini jambo la muhimu ni kuonyesha tuna
vitu gani bora kwa wananchi.”
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye alitoa mada iliyohusu masuala
ya Katiba alisema mchakato wa Katiba hauna budi kurudishwa nyuma kwa
hatua moja hadi kwenye rasimu.
“Kuna
mambo mengi yamejitokeza ambayo yamewachanganya wananchi, hivi sasa
wengi wanatofautiana hawajui uliishia kwenye hatua gani. Pia, hali
iliyojitokeza kule Zanzibar ambapo wakati unajadiliwa awali kulikuwa na
Serikali ya umoja ambayo sasa haipo. Kuna mambo mengi ambayo tumekuwa
tunarudi nyuma hatua tano kisha kwenda mbele hatua mbili.”
Post a Comment