Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
08 Oktoba, 2016 amehutubia katika tamasha la madhehebu ya Bohora ambayo
yanafanya maadhimisho ya dunia ya sikukuu ya mwaka mpya wa Kiislam
Jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yamewaleta nchini wafuasi zaidi ya 30,000 kutoka nchi mbalimbali duniani na kuongozwa na Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb (TUS).
Akihutubia
wafuasi wa Bohora katika Msikiti wa Hakimi uliopo Upanga Jijini Dar es
Salaam, Rais Magufuli amemshukuru Kiongozi Mkuu wa Bohora kwa kukubali
kufanya maadhimisho ya mwaka mpya wa madhehebu hayo hapa nchini na
amewashukuru na kuwapongeza wafuasi wa madhehebu hayo kwa kukubali kuja
hapa nchini na kukaa kwa siku zote za maadhimisho yaani kuanzia tarehe
02 Oktoba, 2016 walipoanza hadi tarehe 11 Oktoba, 2016 watakapomaliza.
Rais
Magufuli, amewapongeza viongozi na wafuasi wa madhehebu ya Bohora kwa
kutumia maadhimisho haya kuhimiza amani, upendo na mshikamano na pia
amewashukuru kwa kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi
ikiwemo mchango Dola za Marekani 53,000 zilizotolewa na Kiongozi Mkuu wa
Bohora kwa Serikali kwa ajili ya kuchangia kampeni ya utengenezaji wa
madawati, na kuwaleta madaktari kutoka Hospitali ya Saifee ya India
waliotoa matibabu bure kwa wananchi wa Arusha.
Aidha,
Rais Magufuli amewakaribisha wafuasi wa Bohora duniani kuja kuwekeza
hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, Uvuvi, Misitu,
Mifugo, Madini na Gesi kwani soko la uhakika lipo ndani ya nchi, katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) yenye watu takribani milioni 400.
Kwa
upande wake Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Dkt. Syedna Mufaddal
Saifuddin Saheb (TUS) amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana na wafuasi
wa madhehebu ya Bohora katika maadhimisho hayo na amesema wafuasi wote
wa Bohora wanahimizwa kushirikiana na mamlaka zilizopo katika nchi
wanazoishi, kuwa raia wema na kufuata sheria.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John pombe Magufuli akiagana na
Kiongozi wa Jumuiya ya Mabohora Duniani, Dk Seydna Mufaddal Saifuddin
kwenye msikiti wa Bohora ulioko Upanga jijini Dar es salaam ambako
alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Mabohora kuadhimisha Mwaka Mpya wa
Kiislamu wa 1438 leo Oktoba 8, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John pombe Magufuli akisalimiana
na Kiongozi wa Jumuiya ya Mabohora Duniani, Dk Seydna Mufaddal
Saifuddin mara alipowasili kwenye msikiti wa Bohora ulioko Upanga jijini
Dar es salaam ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Mabohora
kuadhimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu wa 1438 leo Oktoba 8, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John pombe Magufuli akiwasili
kwenye msikiti wa Bohora ulioko Upanga jijini Dar es salaam ambako
alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Mabohora kuadhimisha Mwaka Mpya wa
Kiislamu wa 1438 leo Oktoba 8, 2016
Post a Comment