Walimu
wanne wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere waliohusika kumpiga vibaya mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Mbeya wamefukuzwa chuo huku Jeshi la Polisi mkoani Mbeya
likiwashikilia kwa mahojiano walimu wengine watano wa shule hiyo
kutokana na tukio hilo.
Aidha,
serikali imemvua madaraka Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kwa
kutochukua hatua baada ya kitendo hicho kufanyika shuleni hapo Septemba
28, mwaka huu.
Hatua
hizo zimechukuliwa baada ya jana katika mitandao ya kijamii kusambaa
kipande cha video kikionesha walimu zaidi ya watatu wakiwa eneo la ofisi
wakimshambulia kwa kumpiga makofi, mateke na fimbo sehemu mbalimbali za
mwili hasa kichwani mwanafunzi Sebastian Chinguku.
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi hao walioshiriki
kitendo cha kumpiga mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu wa Shule ya kutwa
ya Sekondari ya Mbeya.
Walimu
hao ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi huyo kwa
makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa Duce na Evans Sanga
wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza
na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako
alisema kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na kuwa walimu hao
wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua
zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Profesa
Ndalichako alisema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo
kilichofanywa na walimu wanafunzi hao ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi
kufumbiwa macho.
Alitoa
onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo na
kwenda kinyume cha taaluma yao kuwa wanapoteza sifa hivyo amewataka
kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazosomea.
Mkoani
Mbeya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Dhahiri Kidavashari alisema
wanawashikilia walimu wa shule hiyo watano kwa mahojiano kuhusu tukio
hilo. Hata hivyo, alisema si kwamba walimu hao wanaohojiwa ndio
waliohusika na tukio hilo bali wameanza na wale waliopo ili kupata
taarifa zaidi.
“Hatuwezi
kusema sasa hivi kama wale walimu ndio walioonekana katika kipande cha
video kinachosambaa mitandaoni kwa kuwa hili ni suala la mahojiano,
tunaamini hawa tulionao wanaweza wakatupa mwanga,” alisema.
Akieleza
sababu ya adhabu hiyo, Kamanda alisema katika mahojiano ya awali
imebainika kuwa mwalimu wa Kiingereza alitoa kazi, lakini baadhi ya
wanafunzi hawakufanya baadaye mwalimu huyo aliwapa adhabu ya kupiga
magoti, lakini mwanafunzi huyo alionekana kupinga kwa kueleza ana tatizo
la goti hatoweza kufanya adhabu hiyo na mwalimu aliamua kumpeleka
ofisini na kumpiga kwa kumchangia.
“Mwalimu
aliwaadhibu wanafunzi darasani na alipotaka kumuadhibu mwanafunzi huyo
mbele ya darasa, alionesha kupinga kupigwa mbele ya wanafunzi wenzake
ndipo alipoamua kumpeleka ofisini na kutokea tukio linalosambaa,” aliongeza Kidavashari.
Katika
taarifa yake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,
alisema Septemba 28 mwaka huu, mwanafunzi Chinguku wa kidato cha tatu wa
Shule ya Sekondari Mbeya, mkazi wa Uyole, alipigwa na walimu watatu.
“Nimeelekeza vyombo vya dola Dar es Salaam wawatafute chuoni kwao hao walimu kuhusiana na shambulio hilo kwa mwanafunzi huyo,” ilisema Mwigulu.
Naye
Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene ameagiza mamlaka za nidhamu kumvua
madaraka Mkuu wa Shule hiyo, Haule kwa kushindwa kuchukua hatua na kutoa
taarifa mara baada ya tukio hilo kufanywa na walimu hao shuleni hapo.
"Kwa
kuwa waliotenda kosa hili wametoweka tangu Septemba 29, 2016 na
hawajulikani walipo, nimesikitishwa kwa kitendo cha mwalimu mkuu wa
shule hiyo, Magreth Haule kutochukua hatua. Hii inaonesha kulikuwa na
dalili za kutaka kulificha tukio hili baya.
“Na
kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba wanaendelea kuhojiwa na Polisi,
naagiza mamlaka yake ya nidhamu kumvua madaraka mkuu huyo wa shule," alisema Simbachawene katika taarifa yake kwa umma jana.
Katika
hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba
amelaani kitendo kilichofanywa na walimu hao na kukieleza kuwa ni cha
mwituni na cha kinyama kwa kuwa hakuna adhabu kama hiyo katika utumishi
wa ualimu.
"Nami
nimeona hiyo video katika mitandao ya kijamii, kuna sheria za adhabu za
viboko lakini si hii walioifanya hao walimu vijana maana walikuwa
wakipiga makofi, ngumi, mateke, ngwara. Hizi hazipo kwenye ualimu,
lazima wafuate sheria zinazosimamia utumishi wa walimu," alisema Mukoba.
Alishauri
vyuo vya ualimu viweke mkazo katika kufundisha walimu vijana namna ya
kuwa zaidi ya walimu, kuwa na uvumilivu, subira na kuzingatia sheria.
Wafunzwe kisaikolojia kukubali kuwa hawaishii kuwa walimu bali wanaingia
kwenye kundi la malezi.
Alisema
kwa tukio hilo, ni lazima sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho
kwa wengine wenye tabia hizo hasa walimu vijana kwa kuwa kitaaluma ni
tukio la kinyama lisilokubalika.
“Hata kama mwanafunzi ana makosa, amevuta bangi, huwezi kumuadhibu vile, maana pale hujui nani kavuta bangi nani mzima,” alisema Mukoba.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema serikali inalifuatilia kwa
karibu tukio la kupigwa kama mwizi mwanafunzi huyo wa shule hiyo ya
jijini Mbeya na kusema tayari baadhi ya walimu akiwemo mkuu wa shule,
wanashikiliwa na Polisi.
Makalla
alibainisha hayo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe
Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya na kusisitiza kuwa walimu
waliohusika na tukio la kumpiga mwanafunzi wao kama mwizi wanasakwa na
lazima watapatikana.
Alisema
Septemba 26, mwaka huu, mwalimu aliyekuwa katika mafunzo kwa vitendo
katika shule ya Sekondari ya Mbeya Day aliyemtaja kwa jina la Frank
Msigwa alitoa kazi kwa wanafunzi darasani na Septemba 28 alipokuwa
akisahihisha kazi zilizofanyika alibaini baadhi ya wanafunzi
hawakufanya.
Makalla
alifafanua kuwa miongoni mwa wanafunzi aliobaini hawakufanya kazi yake
ni pamoja na Chinguku na ndipo aliwatoa nje ya darasa na kuwapa adhabu
ya kupiga 'push up' lakini mwanafunzi huyo akagoma akidai kuwa na
matatizo ya kiafya katika mbavu zake.
Alisema
baada ya kugomea adhabu hiyo mwalimu aliwaamuru wapige magoti lakini
pia mwanafunzi huyo aligoma akisema ana matatizo ya goti katika moja ya
miguu yake ndipo mwalimu alilazimika kutoa adhabu ya kuwachapa viboko
viwili kila mmoja na aliwapiga wote isipokuwa Chunguku ambaye kama
alivyofanya kwenye adhabu za kwanza hii pia alikataa.
Alisema
baada ya hapo mwalimu huyo alilazimika kwenda kuwaita wenzake wawili
ambao nao walikuwa kwenye mafunzo ya ualimu kwa vitendo shuleni hapo na
wakambeba mwanafunzi huyo hadi ofisini kwao ambako huko ndiko walianza
kumchapa kwa kumchangia kama inavyooneshwa kwenye kipande cha video
kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa
mujibu wa Makalla, walimu waliotenda kitendo hicho walitoroka na
hawajulikani walipo. Alisema serikali inaendelea kuwasaka huku walimu
wengine wakihojiwa Polisi.
Post a Comment