WAZIRI
Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amekiri kuwapo na ugumu wa kufanya siasa
nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka wanachama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujitoa na kufanya kazi kwa moyo.
Sumaye
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitoa kauli hiyo Wilaya
ya Mkuranga, mkoani Pwani jana wakati wa shughuli ya kuchangia ujenzi wa
Ofisi ya Chadema iliyopo wilayani humo.
Alisema
wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya chini wanapaswa kujitoa
katika shughuli za ujenzi wa chama ili kuweza kufikia lengo la kushika
dola ifikapo mwaka 2020.
“Ninaamini
wote tuliopo tutajitoa kwa moyo mmoja, najua ni kazi ngumu kuwa na
chama tofauti na chama tawala lakini tunapaswa kupambana kufikia
malengo,” alisema.
Sumaye
ambaye kabla ya kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka
jana hazijaanza alijitoa CCM na kuhamia Chadema kwenda kumwongezea nguvu
aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alisema kwa
sasa hata CCM inajua kuwa Chadema itashika dola hivyo vijana wakijenge
kuanzia ngazi ya matawi.
“Lazima
tujitolee, dola haipatikani kiurahisi, tunapaswa tuwaeleze wananchi
tutawafanyia nini, hatuwezi kufanya kazi za chama kwenye nyumba ya mtu
au ofisi za vichochoroni kuanzia mwaka 1992,” alisema Sumaye.
Naye
Katibu Mkuu Taifa wa Chadema, Vicent Mashinji, alisema kwa sasa ni
wakati wa kudai Katiba Pendekezwa iliyokuwa ikisimamiwa na Jaji mstaafu
Joseph Warioba, ili kupunguza madaraka ya rais.
“Tunahitaji
Katiba ya wananchi, tunapaswa kufanya hii kampeni kwa ngazi ya msingi,
tunahitaji rais hatuitaji Mungu, rais asiseme mimi sichezewi kwa sababu
yeye si Mungu, ambaye hachezewi ni Mungu tu binadamu wote kuna aina ya
kuchezeana,” alisema Mashinji.
Pia
alisema Katiba mpya itasaidia kupata tume huru ya uchaguzi huku
akirejea uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar Machi 21, mwaka huu na
kudai kuwa Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kukurupuka bila kufuata
sheria za nchi.
“Siamini
kama miaka yote tutavumilia, uvumilivu una kikomo, tunalalamika lakini
inawezekana safari ijayo wakalalamika wao, kila siku mnasema hatushindi
tutashinda tu,” alisema Mashinji.
Alisema kwa mwenendo wa Serikali iliyopo bila Katiba mpya nchi inaweza ikaingia katika machafuko bila sababu za msingi.
Mashinji alisema Taifa linabomoka kuanzia juu kwenda chini na itakuwa ngumu kuliokoa.
Alisema katika uongozi demokrasia ni suala la msingi na si kuongoza nchi kwa matamko na amri.
Katika
hafla hiyo, jumla ya Sh milioni 9.9 zilipatikana ikiwamo ahadi na kati
ya hizo Sh milioni tatu zilitolewa na Dk. Mashinji.
Post a Comment