Mawakili wa Mbunge wa
Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye yupo mahabusu
katika Gereza kuu la Kisongo, jana walishindwa kukamilisha taratibu za
kisheria za kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu .
Wakili wa Lema, John Mallya jana alisema watawasilisha maombi
hayo leo wakati wa kusikilizwa kesi nyingine za mteja wao. “Bado kuna
taratibu zinaendelea na tunatarajia kesho (leo) tutazikamilisha,”
alisema Mallya.
Katibu wa Mbunge Lema, Innocent Kisayegi, alisema baadhi
ya mawakili wa Lema walikuwa na kikao cha kisheria kujipanga kwa kesi
ya leo huku wakisubiri timu nyingine ya mawakili kutoka makao makuu ya
Chadema jijini Dar es Salaam.
“Muda huu leo (jana) mawakili wanaendelea
na kikao na tuna imani leo watakuwa tayari kwa utetezi wa Lema,”
alisema.
Mawakili wa Lema ambao jana walikutana ni James Lyatuu, Sheck
Mfinanga na Charles Aidieli na wanatarajia kuungana na mawakili wengine
akiwamo Mallya.
Hata hivyo, Kisayegi aliwataka wakazi wa Arusha
wajitokeze mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili mbunge huyo na mkewe.
Lema anakabiliwa na mashtaka ya kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais
John Magufuli ambayo yanatajwa kusababisha kukosa dhamana kutokana na
rufani ya dhamana yake kuwekewa pingamizi na wanasheria wa Serikali.
Lema na mke wake, pia wanakabiliwa na kesi ya kutuma ujumbe wa uchochezi
dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na shitaka jingine la
kuhamasisha maandamano ya Ukuta Agosti.
Post a Comment