WATU
sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Yusuf (34) aliyewahi kutajwa na Rais
John Magufuli kwa jina la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili,
wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na
biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Washtakiwa
hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam, huku baadhi wakiwa hawajavaa viatu, wakitembea
kwa kuchechemea.
Baada
ya kusomewa mashtaka, upande wa Jamhuri ulidai unatarajia kuwapeleka
washtakiwa hao katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na
Uhujumu Uchumi, maarufu kama “Mahakama ya Mafisadi” kwa ajili ya kuanza
kusikilizwa.
Washtakiwa
hao watapelekwa katika mahakama hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuandaa
maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo ili kesi hiyo ianze
kusikilizwa.
Yusuf
pamoja na wenzake Charles Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro,
Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi
wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46) walisomewa
mashtaka manne mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba.
Akisoma
mashtaka, Wakili wa Serikali Paul Kadushi alidai katika tarehe tofauti
kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga,
Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na
kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye
thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa
na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea
kudai kuwa katika shtaka la pili kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, washtakiwa
wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye
uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya dola za Marekani 30,000 sawa na
Sh milioni 65.4.
Katika
mashtaka mengine, inadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, washtakiwa wakiwa
Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa
kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni
32.7.
Aidha,
Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh
milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Hakimu
Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu mashtaka yao kwa kuwa
mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliiahirisha
hadi Desemba mosi mwaka huu.
Kabla
ya kutoka kwenye chumba cha mahakama, washtakiwa walimuomba hakimu
awape muda waeleze jinsi walivyokamatwa kwa kuwa walipigwa sana. Mpemba
alidai siku aliyokamatwa, alipigwa sana hadi sasa hawezi kusikia vizuri
na viungo vyake vya mwili havina nguvu hivyo aliomba PF3 ili akatibiwe.
Mrutu
alidai kuwa alipigwa hadi wakamng’oa kidole kimoja cha mkononi na
washtakiwa wengine walidai walipigwa mpaka sasa wanashindwa kutembea
vizuri hivyo waliomba wapewe msaada wa kutibiwa.
Hakimu
Simba alisema hawezi kutoa amri ya kutolewa kwa PF3 kwa sababu Magereza
wana zahanati zao na kuna taratibu wanazifuata hivyo wasiwe na wasiwasi
na kama watashindwa kuwatibia, watatafuta utaratibu mwingine wa
kuwapeleka katika hospitali za nje ya Magereza.
Baadhi
ya washtakiwa, waliingia mahakamani hapo wakiwa wanachechemea huku
wakificha sura zao kukwepa kupigwa picha. Washtakiwa wawili hawakuwa na
viatu.
Post a Comment