0
Mahakama  ya Hakimu Mkazi Tanga, imemtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela miaka 25 au kulipa faini ya Sh bilioni 3.7 mfanyabiashara Charles Kijangwa kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.

Kijangwa alihukumiwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cresencia Kisongo, baada ya kuruka dhamana kwa miaka sita. Alishindwa kulipa faini.

Mshtakiwa huyo alikabidhiwa mahakamani hapo baada ya kukamatwa na askari wa kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Lushoto.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Saraji Iboru, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa Kijangwa alikuwa akitafutwa na Serikali kwa muda mrefu tangu mwaka 2010 baada ya kuruka dhamana katika shauri la uhujumu uchumi namba 6/2007.

Mshtakiwa alishtakiwa na wenzake Michael Msuya na Nyaisa Makori ambao walitiwa hatiani na mahakama, wakahukumiwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la kumiliki kilo 5,000 za meno ya tembo kwa shtaka la kwanza.

Katika shtaka la pili la kula njama, washtakiwa wote walihukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh 10,950,000 baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 5,000 za meno ya tembo kwenda nchini Taiwan mwaka 2006.

Iboru aliiambia mahakama kuwa washtakiwa watatu, Kijangwa na wenzake walihukumiwa kwenda jela miaka mitano au faini ya Sh 50,000 katika shtaka la kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Alidai mshtakiwa hakufika mwenyewe mahakamani hapo bali aliletwa baada ya kukamatwa Desemba 11, mwaka huu wilayani Lushoto.

Aliiomba mahakama kumtia hatiani mshtakiwa na kuhakiksha anatumikia adhabu iliyotolewa dhidi yake akiwa hayupo.

Hakimu Kisongo baada ya kusikiliza maombi hayo, alimtia hatiani mshtakiwa na kumuhukumu kwenda jela miaka 25 au kulipa faini ya Sh bilioni 3.7.

Mshtakiwa Kijangwa alitenda kosa hilo Novemba 2005 na Aprili 2006 kwa kusafirisha makontena mawili ya meno ya tembo yenye ujazo wa tani 5,000 yaliyokamatwa katika bandari ndogo ya Konshugi nchini Taiwan.

Makontena hayo ambayo yalitokea katika Bandari ya Tanga yakiwa na shehena ya kamba za katani na meno ya tembo ndani yake, yalikuwa yanapelekwa Manila nchini Philipine.

Post a Comment

 
Top