0
Kiharusi au kwa Kiingereza Stroke ni kitendo cha baadhi ya viungo vya mwili kuwa na ganzi au kutojiweza kufanya kazi zake za kawaida.Kuna aina mbili za kiharusi, lakini kabla ya kuchambua hayo tuangalie, ni nini kinasababisha mtu kukumbwa na ugonjwa huu?

Mtu anaweza kupata dalili za ugonjwa huu wa kiharusi na baada ya dakika chake zikaisha.
Kiharusi kinampata binadamu baada ya eneo la ubongo kukosa damu kwa saa 24 ama zaidi au kunapotokea kizuizi cha damu au mishipa ya damu kushindwa kusafirisha damu au mshipa huo unapopasuka.

Kiharusi kimegawanyika katika aina kuu mbili kulingana na jinsi kinavyotokea, kwanza ni:
1. Kiharusi cha kukosa hewa kwenye ubongo kitaalamu huitwa Ischemic stroke. (Ischemic ni neno la Kigiriki lenye maana ya kuzuia damu).

Aina hii ya kiharusi hutokea iwapo usambazaji wa damu katika sehemu ya ubongo hupungua na kusababisha tishu za ubongo za eneo lililoathirika kushindwa kufanya kazi zake vizuri.

Hiki hutokea baada ya mshipa wa ateri kuziba kutokana na kuganda kwa damu, hali ambayo inasababisha damu isisafiri vyema na kuelekea kwenye ubongo.

Hali hiyo pia hufanya damu iliyoganda kuziba mishipa midogo ndani ya ubongo  kitaalamu huitwa Cerebral thrombosis au kipande cha damu kumeguka na kwenda kuziba mshipa wa damu kwenye ubongo kitaalamu huitwa Cerebral embolism.

Lakini tatizo hili linaweza kutokea pale damu inapoganda sehemu nyingine ya mwili na kusafiri hadi kwenye mishipa ya ateri, hivyo kusababisha damu kwenda kwenye ubongo kukwama.

Hata hivyo, tatizo hili linaweza kusababisha  kitu kinachoitwa Lacunar stroke, yaani vimirija vidogovidogo sana vya damu vilivyopo ndani ya ubongo, vinaziba.

Hapo sasa binadamu huwa anakumbwa na kiharusi kinachojulikana kitaalamu Lacunar stroke japokuwa mara nyingi hii haiwaletei sana shida wagonjwa.

KIHARUSI CHA HAEMORRHAGE
Baada ya kufafanua kiharusi kinachoitwa ischaemia ambacho ndani yake tukaelezea pia kile kinachoitwa Lacunar stroke, sasa tuelezee aina ya kiharusi kiitwacho Haemorrhage.

Aina hii ya kiharusi, mrija wa damu karibu ama kwenye ubongo hupata mpasuko, hivyo kusababisha damu kuvuja na kitendo hicho ndicho kitaalamu huitwa Haemorrhage.

Kinachotokea ni kwamba damu inayovuja hukandamiza ubongo na kuuharibu, ubongo ni moja ya kiungo laini sana mwilini.

Katika hali ya kitaalamu inayoitwa Intra cerebral haemorrhage, uvujaji wa damu hufanyika ndani ya ubongo wenyewe. Mara nyingi aina hii ya kiharusi hutanguliwa na dalili za kichwa kuuma, au kuwepo kwa historia ya ajali ya kichwa.

Lakini kuna hali pia inayoitwa Subarachnoid haemorrhage ambapo mpasuko wa mshipa wa damu hufanyika karibu na eneo linalozunguka ubongo linaloitwa Subarachnoid.

Wakati fulani, mishipa ya damu huzungukwa na aina fulani za mafuta yasiyofaa mwilini, hali inayoitwa kitaalamu kama Atherosclerotic plaque. Hali hii husababisha kuganda kwa damu katika mishipa (thrombosis) hiyo.

Iwapo mgonjwa ataathirika sehemu ya ubongo kwenye shingo kuelekea kwenye uti wa mgongo (brainstem), mgonjwa anaweza kuwa na dalili za kuhisi mabadiliko ya harufu, ladha, kusikia na  kuona, kulegea kwa misuli ya macho (ptosis),  kupungua kwa ufahamu na kulegea kwa misuli ya uso, ulegevu wa ulimi (kushindwa kutoa nje au kusogeza upande upande).

Pia atakuwa na upungufu wa uwezo wa kumeza, ulegevu wa misuli ya shingo na kushindwa kugeuza shingo upande mmoja, kushindwa kusimama sawasawa na kuona vitu kwa hali ya utofauti, mabadiliko ya upumuaji na kiwango cha moyo kudunda.

Iwapo sehemu mojawapo ya mfumo mkuu wa neva kitaalamu huitwa central nervous system  imeathirika, mgonjwa atakuwa na dalili za kupoteza ufahamu kwa upande mmoja wa mwili na kulegea kwa misuli ya uso, kuhisi ganzi mwilini na kupungua kwa ufahamu wa hisia na kutetemeka mwili.

Mgonjwa anaweza kukumbwa na matatizo ya kupoteza fahamu, maumivu makali ya kichwa na kutapika hasa kwa wale wenye kiharusi cha kuvuja damu (hemorrhagic stroke) ambacho husababisha ongezeko la shinikizo na mgandamizo wa ubongo ndani ya fuvu kutokana na kuvuja kwa damu.

TIBA
Mgonjwa kabla ya kutibiwa ni lazima afanyiwe vipimo kama vile cha ECG, ECHOCARDIOGRAM  ambacho huwezesha kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo ( na kama kuna damu iliyoganda kwenye moyo ambayo inaweza kufika kwenye ubongo.

Holter monitor husaidia kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo (arrhythmia) zinazotokea kwa vipindi na Angiogram huwezesha kugundua matatizo kwenye mishipa ya damu, na ni mishipa ipi ya damu iliyoziba.

Vipimo vya damu huwezesha kutambua uwepo wa lijamu mwilini (hypercholesterolemia) na mabadiliko mengine katika damu.

Mgonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za kuyeyusha damu iliyoganda (thrombolytics) au kwa kuondoa damu iliyoganda kwa njia mbalimbali (thrombectomy). Dawa nyingine kama vile junior Aspirin na Clopidogrel hutolewa kwa ajili ya kuzuia chembe sahani kukusanyika na kuganda.

Matibabu ya kiharusi kinachotokana na damu kuvujia kwenye ubongo (Hemorrhagic stroke)  huhitaji tathmini ya upasuaji wa neva ili kuchunguza na kutibu sababu ya damu kuvuja. Haishauriwi kabisa kumpa mgonjwa wa aina hii ya kiharusi dawa za kuyeyusha damu iliyoganda au za kuzuia kuganda maana huhatarisha maisha ya mgonjwa badala ya kumsaidia. Kwahiyo ni vizuri kwa wataalamu kufanya uchunguzi wa kutosha ili kuwa na uhakika na tatizo.

Mgonjwa wa kiharusi inafaa kumuelimisha ili arudishe ujuzi wake wa maisha ya kila siku. Inashauriwa wataalamu wa viungo wanahitajika ili kumpa mazoezi mgonjwa.

Hatari ya ugonjwa huu ni kwamba asilimia 75 ya wanaonusurika kifo huwa walemavu wa akili au kimwili na kusababisha kuathirika kwa ufanyaji kazi wao .

Ulemavu wa kimwili ni pamoja na ulegevu wa misuli, kujihisi ganzi sehemu mbalimbali za mwili hususan zilizoathirika, kutoona vizuri, vichomi na kadhalika.

USHAURI
Wagonjwa wanashauriwa kutibu au kuzuia tatizo la shinikizo la damu, kisukari na wanapewa ushauri wa kufanya mazoezi kila siku, kuacha kuvuta au kunywa pombe kupita kiasi, kula chakula kisichokuwa na mafuta mengi na kisicho na chumvi nyingi.

Tumia dawa za kupunguza mafuta mwilini (statins) kwa mfano Simvastatin.
Watu waepuke unene kupita kiasi (obesity) na wajichunge wasipate  cholesterol nyingi kwenye damu ambayo huchangia kuziba kwa mishipa ya damu mwilini.

Post a Comment

 
Top