0

rais-maduroRAIS Nicolous Maduro Moros, ana vibweka visivyohusiana na wadhifa wake kutokana na anavyoiongoza Venezuela kwa mkono wa chuma, licha ya kurithi nafasi hiyo kutoka kwa Rais mwenye msimamo mkali uliotikisa mataifa ya nje Hayati Hugo Chaves.
Awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo chini ya utawala wa mtangulizi wake, pia akiwa Makamu wa Rais katika kipindi cha miaka saba aliyoshikilia nyadhifa hizo kwa pamoja. Maduro aliyewahi kuwa dereva wa mabasi ya abiria kabla hajawa kiongozi wa chama cha wafanyakazi nchini Venezuela, alikaimu madaraka baada ya kifo cha Chavez.
Baadaye alishinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka mmoja tangu Chavez afariki dunia mnamo mwaka 2013. Kwa wasifu wake huyu ni mtu aliyetokea kuendesha mabasi, hadi kupanda kuwa Rais wa nchi hiyo ameshindwa kuendeleza mashiko ya mtangulizi wake.
Kutokana na mfumo wake tatanishi wa kuongoza amesababisha taifa hilo kuyumba kiuchumi kwa mfumuko wa bei kuongezeka, uhalifu kuzidi maradufu, umasikini na baa la njaa pamoja na ukosefu wa bidhaa muhimu kwa maisha ya binadamu hata za kawaida tu ambazo haziathiriwi na myumbo wa uchumi, nazo zimekuwa na uadimu mkubwa ikiwemo karatasi za msalani (toilet papers).
Majeneza ya kuzikia kutokana na mgawo endelevu wa umeme hivyo hakuna uwezekano wa kukata miti ambayo ni ghafi muhimu ya kutengenezea. Kuna wakati wananchi wa Venezuela walilazimika kurudia mfumo wa kijadi wa uzikaji kwa kutumia mikeka kwa kuchimba makaburi yenye kizimba cha kumweka marehemu (kimwana ndani), kutokana na ukosefu wa majeneza kwa athari kubwa ya kiuchumi iliyolikumba taifa hilo.
Mkanganyiko mwingine kumhusu Rais Maduro ni hulka yake ya kusingizia mataifa ya kigeni unapotokea mbinyo kutokana na staili yake ya kuongoza, pia kufanya matendo yanayotafsiriwa kama kebehi na kudharau mwenendo usioridhisha wa taifa hilo.
Katika moja ya hotuba zake aliwahi kuwaambia wanawake nchini humo wenye kawaida ya kufuga nywele ndefu, waache kutumia vikaushia nywele (hair driers) kwa kuwa wanatumia umeme mwingi wakati taifa linapitia katika mgawo.
Kutokana na hali hiyo, Venezuela imekuwa nchi ya migomo na maandamano na wapinzani wanajaribu kila mara kumng’oa madarakani bila mafanikio, Rais Maduro akitumia Mahakama Kuu na tume ya uchaguzi kujikinga lakini wapinzani wakipiga hatua na kufanikiwa kukamata Bunge kwa wingi wa wawakilishi, wakitarajia kumdhoofisha kupitia miswada ya Serikali inayowasilishwa bungeni ingawa inavyoelekea safari ya kumtoa madarakani bado ni ndefu na ngumu kukamilika hadi kufikia mafanikio.
Hivi karibuni Rais huyo mtata amelikoroga tena baada ya kutangaza kusitisha matumizi ya fedha ya ‘Bolivir 100’ ambayo umuhimu wake kwa watu wengi kwenye manunuzi ya bidhaa ni mkubwa kutokana na uwezo wao kimaisha, kitendo kilichosababisha kuzuka kwa ghasia kutokana na wauzaji kuzikataa fedha hizo na kusababisha wananchi wateseke kwa kukosa huduma muhimu hata kununua chakula cha kujikimu.
Wakati Maduro anatangaza kuiharamisha noti hiyo tayari ilishaanguka thamani yake katika soko, lakini ndiyo noti inayotumika zaidi na watu wengi katika manunuzi ya kila siku huku mwenyewe akijitetea kuwa hatua hiyo ilidhamiria kuzuia utakatishaji fedha unaofanywa na magenge ya mafia mipakani mwa nchi hiyo na kuidhoofisha kiuchumi Venezuela licha ya kuwa mojawapo ya mataifa yanayouza mafuta duniani.
Kwa hatua hiyo ya ghafla ATM za nchi hiyo zimekauka na mabenki hayapokei fedha mpya zilizoahidiwa kuanza kutumika kama mbadala wa noti hiyo iliyotangazwa kuondolewa katika mzunguko.
Kama kawaida yake Rais Maduro akayashutumu mataifa ya kigeni kwa kusababisha uchelewaji wa noti mpya kuwasili nchini mwake kwa njama za kuihujumu Serikali yake, lakini wananchi wake hawakumwelewa na kuamua kuandamana na kuvunja maduka kuiba bidhaa muhimu walizozikosa kutokana na kutokubaliwa kwa noti hiyo aliyotangaza kuiharamisha.
Licha ya kutangaza kusitisha kwa muda zoezi hilo, lakini bado hamkani si shwari katika taifa hilo ambalo uchumi wake unayumba na unaporomoka kwa kasi hususani katika kipindi cha utawala wa Rais huyo.
Lakini katika hulka yake ya kushangaza, Maduro akatangaza mafanikio kwamba asilimia ya benki nchini mwake kumiliki noti hizo imeongezeka na kuzipa nguvu zaidi ya soko, kutoka asilimia 2 hadi 80.
Lakini kwa vituko vya Rais huyo kwa wanaomfahamu haikushangaza kwa kuwa majuma machache yaliyopita, akiwa na mkewe katika mkutano na waandishi wa habari aliinuka ghafla na kuamuru muziki wa rhumba upigwe naye akaanza kusakata muziki na mkewe, akionesha ufundi mkubwa na kudai kuwa maisha ni mazuri nchini humo ndiyo maana anaweza hata kucheza muziki kwa ufundi, lakini uhakika ni kuwa Venezuela inazidi kutumbukia katika ombwe la sintofahamu kuhusiana na mustakabali wake.
Katika hatua nyingine Rais huyo ameongeza muda wa kufunga mpaka na Colombia wanakokimbilia wananchi wake kujipatia bidhaa, tayari Colombia inamshutumu mcheza rhumba huyo kwa uchokozi unaodhoofisha uhusiano wa mataifa hayo mawili, kwa kuwa kwa sasa amani imetamalaki Colombia kwa Serikali na kundi la waasi la wapiganaji wa FARC kusitisha mapambano.

Post a Comment

 
Top