0
MANCHESTER, England
MANCHESTER United hawajafungwa michezo 7 mfululizo ya Premier League, katika mechi vitasa, Marcos Rojo na Phil Jones, walizocheza pamoja.
Na katika michezo hiyo, wameokoa kwa pamoja mashambulizi 139 yaliyokuwa yakielekea langoni kwao, wanapiga kazi kweli kweli!
Lakini amini usiamini, kabla ya Oktoba 23, mwaka huu si Marcos Rojo au Phil Jones aliyekuwa na ndoto ya kucheza kikosi cha kwanza, siku zao ndani ya Old Trafford zilianza kuhesabika.
Lakini kuumia kwa Eric Bailly na kiwango kibovu kilichoonyeshwa na Chris Smalling kwenye kichapo cha bao 4-0 mbele ya Chelsea, vikatosha kuwa sababu mbili kwa Jose Mourinho kuwapa nafasi wawili hawa.
Viwango vyao vikaimarika na kutengeneza ukuta mgumu ulioisaidia United kurudi kwenye mstari na kuanza kupata matokeo.
Na umoja wao ukampa shida Jose Mourinho ambao licha ya kurejea kwa Eric Bailly, bado alishindwa namna ya kuwapangua Rojo na Jones katika ngome yake ya ulinzi.
Kwa kuangalia ubora wa beki mmoja mmoja, Rojo anashika namba moja kwa kuwa na wastani wa 10.41 wa kuokoa hatari langoni kwake, huku Jones akifuatia akiwa na 10.2.
Idadi hii ni kubwa kulinganisha na Smalling mwenye wastani wa 7.84, Bailly (6.31) na Blind (5.7).
Uimara wa Jones na Rojo umekuja baada ya wawili hawa kuwa na ushirikiano mkubwa wa kusaidiana majukumu ya kukaba na si kutegeana.
Awali ilionekana ngumu sana lakini Mourinho aliwaamini na kuhakikisha Rojo aliyezoeleka kucheza kama beki wa kushoto, akiingia katikati na kuonyesha ukomavu wake.
Faida nyingine ya wawili hawa ni uwezo wao wa kumiliki mpira unaowafanya viungo wa United wanaoongozwa na mkongwe, Michael Carrick kuwa na kazi rahisi ya kutengeneza mashambulizi kutoka nyuma ya uwanja.
Bao la Henrikh Mkhitaryan dhidi ya Tottenham ni mfano wa haraka wa kuonyesha ushirikiano uliopo katika kikosi cha United kutoka nyuma mpaka mbele.
Ni rahisi kuona kazi kubwa ya Carrick na Herrera katikati ya uwanja ikiwa Rojo na Jones wanafanya kazi yao kwa ufasaha mkubwa.
Pia wawili hawa wamekuwa faida kwa David de Gea ambaye katika misimu ya hivi karibuni alikuwa na kazi kubwa ya kuiokoa United kwa kuokoa michomo mingi iliyokuwa ikielekezwa langoni mwake.
Lakini pia wachambuzi wengi wa soka nchini England wanasema kuwa utulivu wa Michael Carrick unawapa nafasi kubwa Rojo na Jones kujiamini na kufanya majukumu yao ya ukabaji tu uwanjani.
Herrera na Carrick wanaonekana kuibalansi vyema United katikati ya uwanja na kuipa nafasi beki zao za kati kutulia na kusoma mashambulizi ya wapinzani yanapoanzia na kuyazuia.
Hii ni faida kwa United ambao kwa sasa watakuwa na hazina ya mabeki wa kati watatu bora kwenye kikosi chao hivyo kuwa na uhakika wa kufanya vyema kwenye michuano mbalimbali wanayoshiriki msimu huu.

Post a Comment

 
Top