Baadhi ya vifungu katika sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari
vimebainika kuwa vinaweza kuchochea baadhi ya makampuni kushiriki katika
mbinu chafu za kibiashara ikiwemo ukwepaji wa kodi.
Hali hiyo inatokana na vifungu hivyo kudhoofisha uandishi wa habari za
kiuchunguzi, hasa zile zinazolenga kufichua uovu unaofanywa na makampuni
hayo.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Wakili Mwandishi Bw.
James Marenga, wakati wa mjadala wa wanahabari kuhusu sheria mpya ya
huduma za vyombo vya habari, mjadala ulioandaliwa na ya taasisi ya
habari ya Kimataifa ya Internews, kwa lengo la kuwapa waandishi nchini
uelewa mpana wa maudhui ya sheria hiyo.
Serikali katika mjadala huo iliwakilishwa na Kaimu Msajili wa Magazeti
Bw. Patrick Kipangula ambaye amesifu baadhi ya vifungu katika sheria
hiyo kwa maelezo kuwa vitaboresha tasnia ya habari pamoja na maslahi ya
waandishi wa habari nchini.
Awali katika maelezo yake, Mwezeshaji kutoka Internews na Mwandishi
Mkongwe Bi. Alakok Mayombo amesema mjadala huo umelenga kuwawezesha
wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria hiyo pasipo
kusuguana na serikali sanjari na kutoa mwanya wa kufanyia mabadiliko
baadhi ya maeneo yanayoonekana kikwazo kwa kazi ya uandishi wa habari.
Post a Comment