WACHEZAJI wa Yanga, jana walifanya mgomo wa mazoezi
asubuhi wakiushinikiza uongozi wa timu yao kuwalipa
mishahara yao ya mwezi Novemba.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, mmoja wa vigogo wa Yanga, ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini, alisema wachezaji wote walifika uwanjani hapo saa tatu na
nusu asubuhi.
Alisema
baada ya kuwasili kwenye uwanja huo, waligoma kubadili nguo na kuvaa za
mazoezi huku wakisisitiza kuwa hawatafanya mazoezi hadi hapo uongozi
utakapowalipa mishahara yao.
Alisema
licha ya Kocha George Lwandamina kutoka Zambia, kuwasihi wafanye mazoezi
angalau kwa muda wa nusu saa, wachezaji hao walimuwekea ngumu na
kumwambia msimamo wao upo pale pale hadi hapo watakapolipwa mishahara
yao.
“Jumatatu
iliyopita waligoma kuingia kambini kwa sababu hii hii, lakini tuliwasihi
wasitishe mgomo ili wajiandae na mchezo wetu dhidi ya JKT Ruvu walikubali.
“Tulicheza
dhidi ya JKT Ruvu kwa morali ingawa tulikuwa na wasiwasi kuwa huenda wakaharibu kwenye mchezo ule, lakini
tulishukuru waliingia uwanjani na kucheza kwa moyo mmoja na ndio maana
tulifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-0,”alisema kiongozi huyo.
Alisema
wachezaji walitegemea baada ya mchezo huo wangerekebishiwa madai yao, hali
ambayo haijatekelezwa hadi sasa.
Alisema anadhani wachezaji hao wameona ufumbuzi wa suala hilo ni kutofanya
mazoezi na kuendelea na mgomo wao.
Kutokana na
mgomo huo, benchi la ufundi la Yanga lilifanya jitihada za kuwasiliana na
uongozi ili kuona wanatatua vipi tatizo hilo ili
wachezaji hao warejee kwenye morali ya kufanya mazoezi.
“Hadi sasa
bado hatujajua suala hili litaisha muda gani, kama ni leo (jana) au kesho (leo),
tunawasiliana na viongozi tujue tunafanyaje,”alisema.
Wachezaji
wote wa Yanga walitimka uwanjani hapo ilipofika saa 4:30 na kurejea
majumbani mwao kusubiri mustakabali wa madai yao.
Yanga ipo
nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikijikusanyia pointi 36
huku Simba ikiwa kileleni mwa ligi kwa kuwa na pointi 38.
Baada ya
mchezo wao na African Lyon, Yanga itasafiri kwenda visiwani Zanzibar, kucheza
michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo Yanga itaanza kurusha karata yake ya
kwanza dhidi ya Jamhuri, mchezo utakaopigwa Januari 2 saa mbili usiku.
Post a Comment