0
MAAFISA Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kuacha kutumia muda mwingi kukaa maofisini na badala yake kutembelea jamii inayowazunguka ili kubaini fursa zitakazoleta mabadiliko ya haraka katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Sihaba Nkinga wakati wa mahojiano Maalum ya kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa hewani na Shirika la Utangazaji Nchini (TBC).

Bi. Sihaba amesema kuwa Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuanzisha Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuzalisha maafisa wengi wa kada hiyo watakaotumika kuisaidia Serikali katika kuibua fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii ambazo zitasaidia kuleta maendeleo ya nchi.

“Afisa Maendeleo ya Jamii ni chachu ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla kwani wao ndio wana jukumu la kubaini fursa na kuwaongoza wananchi katika kutumia fursa hizo,” alisema Bi. Sihaba.

Ameongeza kuwa jukumu kubwa la maafisa maendeleo ni kuwahamasisha, kuwashirikisha na kuwajengea uwezo wanajamii kutumia rasilimali walizonazo kujiletea maendeleo yatakayopelekea kukua kwa uchumi wa nchi.

Aidha, Bi. Sihaba amewataka wananchi kuacha dhana potofu ya kuitegemea Serikali na badala yake washirikiane na Serikali kuleta maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka katika maeneo wanayoishi.

Akiongelea kuhusu makazi ya wazee, Bi. Sihaba amesema kuwa kwa sasa kuna vituo 17 nchi nzima vyenye jumla ya wazee 460 wanaopatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za malazi, mavazi na chakula.

“Tunatoa rai kwa vijana kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujitegemea na sio kwenda kukaa kwenye nyumba za wazee ili wapatiwe huduma, makazi ya wazee ni kwa ajili ya wazee wasiojiweza tu,” alimalizia Bi. Sihaba.

Post a Comment

 
Top