0
KIUNGO wa zamani wa Yanga anayechezea klabu ya Mbeya City, Mrisho Ngassa amesema kwamba Yanga inahitaji wachezaji wawili wa kuchezesha timu ili kuwa na uwiano mzuri kikosini.
Akizungumza kwenye mahojiano na gazeti hili jana, Ngasa, alisema kuwa Yanga inahitaji wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho.

“Ukiangalia Yanga wanavyocheza kwa sasa, unaona kabisa inakosa watu kama wawili wa kuchezea mpira na kutoa pasi za mwisho kama alivyo Niyonzima (Haruna). Ili wawe na uwiano mzuri katika timu, lazima wawapate hao watu,”alisema.

Maoni hayo ya Ngassa yanafuatia Yanga kufanya vibaya katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa na Simba kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 Jumanne usiku kwenye uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

“Mechi ilikuwa nzuri, Simba waliwazidi katikati Yanga, ambao walikuwa wanacheza mipira mirefu kumtumia Msuva (Simon) peke yake, hivyo Simba wakagundua njia hiyo, baada ya kusogea pembeni wakaua mipango ya Yanga," alisema Ngasa.

Pamoja na hayo, Ngassa alisema kwamba wachezaji wengi wa Yanga kwa sasa wamechoka baada ya kucheza michezo mingi ya kimashindano, hivyo wengi wao miili yao inahitaji kupumzika.

Post a Comment

 
Top