MKUU WA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO YA KLABU YA SIMBA, HAJJI MANARA
SIMBA imepanga kuondoka jijini Dar es Salaam keshokutwa Alhamisi
kuelekea Songea kucheza na Majimaji huku wakiwa na dhamira moja ya
ushindi.
Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu itaenda
Songea huku ikiwa na uchungu wa kutolewa kileleni na wapinzani wao,
Yanga ambao ushindi wao wa mabao 2-0 umewafanya kuwaacha wekundu hao wa
Msimbazi kwa pointi moja baada ya kufikisha pointi 46.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Hajji Manara, alisema wataenda Songea baada ya kucheza mchezo wao wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa Afrika, Mamelodi.
“Mchezo huu wa kesho wa kirafiki kwetu ni sehemu ya maandalizi ya kabla ya kucheza na Majimaji na pia tunatarajiwa kujifunza mengi kutoka kwa wenzetu, ambao ni mabingwa wa Afrika,”alisema Manara.
Alisema wataenda Songea huku wakiamini ni ushindi tu wanaoufuata.
"Kila mmoja wetu ameumia na kitendo cha kupoteza mchezo wetu na Azam na kupelekea kushuka kileleni, tutaenda kupambana kupata ushindi, tunaamini bado tuna nafasi ya kurejea kileleni," aliongeza kusema Manara.
Alisema mashabiki wasiwe na hofu kwa kuwa bado kuna michezo mingi mbele yao ambayo wanaweza wakaitumia kulejea kileleni na hatimaye kutwaa ubingwa msimu huu.
Post a Comment