Taarifa za mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kuitumikia Simba kwa vipindi viwili tofauti na kisha alijiunga na mahasimu wao Young Africans, zimeibuka kufatia kuvunja mkataba na klabu ya Sønderjysk ya nchini Denmark.
Afisa habari wa shirikisho la soka nchini TFF Alfred Lucas amesema mshambuliaji huyo anabanwa na kanuni za usajili wa wachezaji hapa nchini, hivyo hata kama atasajiliwa na Simba hatoweza kucheza katika michezo ambayo inaendeshwa na shirikisho hilo.
“Msimu huu tunaoenda nao duru la pili, usajili wake ulianza June 15 ukaisha August 6, 2017. Dirisha dogo la usajili lilifunguliwa November 15 likafungwa December 15 kwa hiyo suala la usajili wa mtu mnayemtaja Okwi, Simba inaweza ikamsajili lakini itamtunza tu au kucheza mechi za kirafiki,” anasema Alfred Lucas msemaji wa TFF.
“Kucheza mechi za ligi kuu au kombe la FA kwa msimu huu wa January mpaka May au June hatocheza. Kwenye mpira wa miguu ukikosa utaratibu, kanuni au sheria mpira wa miguu hakuna tutakuwa tunafanya mambo ya hovyo-hovyo.”
Kuhusu taarifa ambazo zinazoendelea kusambazwa na afisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara, Alfred Lucas amesema TFF haiwezi kuzuia suala hilo ama kukemea kutokana na uhuru wa mtu mwenyewe kuwa na utamaduni tofauti na kanuni za usajili ambazo zipo wazi.
“Yule amezungumza na mashabiki wake, kama ni kawadanganya au kawaambia ukweli wao wanajua, hajaitukana TFF.”