0
Wanasema mwanamke na mwanaume ni tofauti kwenye baadhi ya mambo, kimaumbile. Lakini, sio yale mambo yenye kuonekana peke yake, kwani imebainika sasa ni kwamba, tofauti huenda hadi kwenye usingizi. Ni kwamba mwanamke na mwanaume huota tofauti.

Kwa hiyo, hata wakiwa usingizini, mwanamke na mwanaume wanaendelea na tofauti zao.
Dk. Mark Blagrove, ambaye ni mtaalamu wa saikolojia, anasema kwamba, yeye pamoja na mwenzake wamefanya utafiti kwa watu zaidi ya 100,000 na kubaini kwamba, kuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume hasa linapokuja suala la kuota ndoto.

Utafiti uliofanywa na Blagrove na wenzake umehusisha watu wa dunia nzima, sio ulaya na marekani peke yake.

Hivyo, ni utafiti ambao unazungumzia jambo linalohusu dunia nzima, siyo upande fulani tu wa dunia.

Katika utafiti huo, wamegundua kwamba, wanandoa ambao wamelala kitanda kimoja, ubavu kwa ubavu, wanakuwa na ndoto tofauti kabisa, ingawa wanaweza wakawa wanaota wakati mmoja.

Ndoto za wanawake zinaonekana wazi zinahusu kazi, zimejaa hisia sana ndani yake na huchukua muda mrefu zaidi.

Mwanamke anaweza kusimulia kuhusu ndoto yake, ukadhani imechukua saa kadhaa kuota kwa jinsi ilivyo ndefu. Huwa wanaota ndoto moja kwa muda mrefu zaidi.

Ndoto za wanawake zimejengwa kwenye msingi wa nyumbani na kuhusisha watu wengi na hasa wa familia zaidi, kuliko watu wa nje ya familia.

Kwa upande wa ndoto za wanaume, kuota wageni ni jambo la kawaida sana kwao. Wageni, ina maana watu ambao hawawafahamu. Ndoto za wanaume zimejengwa kwenye msingi wa maeneo ya barabara, magari na vurugu.

Hauwezi kupita muda mrefu kabla mwanaume hajaota kuhusu gari, barabara au vurugu za aina fulani.

Huhusisha pia tendo la ndoa na wanawake wasiowajua, mara nyingi.
Ndoto za wanaume pia zimejengwa pia kwenye mazingira ya kazi, na kuhusiana na hofu za kipato na hofu za kupoteza kazi au kufilisika. Zimejaa masuala ya kazi au shughuli.

Mwanasaikolojia aliyeandika pia vitabu kadhaa kuhusu ndoto, Veronica Tonay, anasema, utafiti huu unathibitisha tafiti za siku nyingi ambazo zilikuwa zinadai kwamba, wanawake huota tofauti na wanaume.

Hivi sasa, inaweza kusemwa kwamba, suala hilo halina utata tena. Inaonyesha pia kwamba, zaidi ya nusu ya watu wote wanapata ndoto mbaya angalau mara moja kwa wiki.

Kuna wengine ambao ndoto mbaya ni sehemu ya maisha yao ya kindoto,yaani karibu kila siku zinawatokea.

Inaelezwa kwamba, kazi anayofanya mtu inaweza kuchangia kwenye kuwa kwake na ndoto za jinamizi au ndoto mbaya.

Kwa mfano, wauguzi wahasibu na watumishi kwenye vyombo vinavyohusiana na mawasiliano, ndiyo ambao hukumbwa sana na ndoto hizi mbaya.

Soma; Ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuishi na watu hawa.
Kukimbizwa, meno kudondoka, kuanguka, kutegewa au kuwekewa kizuizi, ni miongoni mwa mada zinazootwa sana, hasa na wale wanaoota majinamizi.

Wanasaikolojia wanasema, ndoto zinahusiana na shughuli ambazo hatujazimaliza kwenye mpangilio wetu wa kazi wa siku au kujaribu kufanya kile ambacho tulishindwa kukifanya tukiwa macho.

Kwa mfano, kuota kupata fedha, jambo ambalo katika hali ya kawaida, limekuwa gumu kwetu.
Watafiti hapo wanazidi kuchambua ndoto kwa kusema kwamba, ndoto zinazohusu mambo mabaya ndizo ambazo zinaotwa zaidi kuliko zile zinazohusu mambo mazuri.

Hata wale watu wenye furaha maishani, wanaonekana kuota ndoto zenye mada zisizopendeza kuliko mada zenye kupendeza.

Ingawa wataalamu wa ndoto wanasema, kila ndoto ina maana kutegemea na mtu aliyeota, utafiti huu unaonyesha kwamba, pamoja na kuwa hilo ni kweli, kuna mambo ambayo mtu mmoja akiyaota , maana yake ni ile ile kwa mtu mwingine yeyote.

Kwa mfano, kuanguka, kwenye ndoto ina maana ya mtu kukosa uhakika wa usalama.
Kukimbizwa au kufukuzwa, bila kujali ni nani anaota, inaweza kuwa na maana ya kukimbia matatizo.

Ndoto ya kupoteza au kung’oka meno inahusiana na mtu kujali namna anavoonekana au sura.
Ndoto ya mtu kukimbia, lakini lakini akajikuta bado yupo pale pale, yaani hasogei, ina maana au inahusiana na mtu kuwa na kazi nyingi kumzidi uwezo.

Ndoto ya mtu kuwa uchi, ina maana kwamba, mhusika ana matamanio ya kuwasiliana na mwingine au wengine.

Kile ktiendo cha kuvua nguo ndotoni kina maana ya mtu kuondoa vikwazo vinavomkabili kwenye maisha ake.

Pamoja na kwamba, lengo la utafiti huu lilikuwa ni kuona kama mwanamke na mwanaume wanaota tofauti, bado umezaa masuala mengine muhimu ynayohusiana na ndoto. Moja ya hili lilozaliwa ni maana ya ndoto, ambazo hazibadiliki, bila kujali ni nani ameziota.

Post a Comment

 
Top