0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka leo awapeleke wakaguzi wa heshabu kwenda kukagua mapato na matumizi ya  Mamlaka ya Maji ya Mji wa Njombe (NJUWASA).

Ametoa agizo hilo jana (Ijumaa, Januari 27, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Mpechi, Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Waziri Mkuu alisema wakaguzi hao mbali na kukagua mapato na matumizi ya mamlaka hiyo pia waangalie kama wananchi walihusishwa katika ukokotoaji wa gharama za malipo ya bili za maji.

Alitoa agizo hilo baada ya wananchi kuilalamikia mamlaka hiyo kupitia mabango kwamba wanatozwa bili kubwa ya maji licha ya huduma hiyo kupatikana kwa kusuasua katika mji huo.

Kufuatia malalamiko hayo Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa NJUWASA, Bw. Daudi Majani kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo ambapo alisema kwa mwezi wanakusanya sh. milioni 75 zinazotumika kuendeshea na uboreshaji wa huduma.

“Maji hakuna unasema unaboresha unaboresha huduma gani? Wananchi wanalalamika maji hakuna na mnawatoza gharama kubwa, Mkuu wa Mkoa kesho peleka wakaguzi wakakague kwa mwezi anakusanya kiasi gani na anafanyia nini,”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa umma kujiwekea utaratibu wa kwenda kwa wananchi na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi badala ya kujifungia maofisini.

“Uwepo wa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi ni ishara tosha kwamba watendaji hamuendi kwa wananchi kuwasikiliza kero zao. Mabango mengi hapa si ya Waziri Mkuu ni hapahapa,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Post a Comment

 
Top