Wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye kikao cha pamoja kupinga kunyang’anywa mihuri jana.
Kwa mujibu wa wenyeviti hao, hawatashiriki kwenye shughuli yoyote ya mtaa au kata kama ilivyokuwa awali.
Wenyeviti hao zaidi ya 500, bila kujali itikadi za vyama vyao waliungana na kutoa tamko la kutojishughulisha na utendaji wa aina yoyote kama ilivyokuwa awali.
Mbali na kuapa kutojishughulisha na shughuli zozote za mitaa, vilevile walihimizana kila kiongozi arudishe muhuri bila shuruti ili kuachana na kazi hiyo.
Walikuwa wakizungumza jana katika Ukumbi wa Klabu ya Sigara (TCC), Chang’ombe wilayani Temeke.
Walisisitiza kuwa wao si wenyeviti tena na hawatajihusisha na shughuli zozote za mitaa wala kata.
VIASHIRIA VYA VURUGU
Hata hivyo, wakati wenyeviti hao walipokuwa wanataka kuanza mkutano wao jana, viashiria vya vurugu vilianza kutokea.
Walifika watu waliosadikiwa kuwa ni maofisa usalama na ghafla umeme ulizimwa kwenye ukumbi walimokuwa na hivyo kufanya vipaza sauti vishindwe kufanya kazi.
Watu hao wakiongozwa na OCCID wa Wilaya ya Temeke walifika wakiwa na gari mbili za polisi na Mkuu wa Wilaya, Felix Lyaviva, na muda mfupi baadaye walitoka nje na viongozi wa wenyeviti hao.
Viongozi hao walijadiliana na mkuu huyo wa wilaya ambaye baadaye aliwaacha waendelee na mkutano wao.
Kabla ya kuondoka katika eneo hilo, Lyaviva, aliwahakikishia waandishi wa habari kwamba wamekubaliana na wenyeviti hao warudishe mihuri bila mashariti na wataendelea na majukumu yao kama kawaida.
MSIMAMO WA WENYEVITI
Katibu wa Wenyeviti hao, Mariam Machicha, alisema msimamo wao uko palepale, kwamba hawataendelea na huduma zozote.
Msimamo huo ambao uliwekwa kwenye maandishi, ulisema kuanzia jana hawatafika katika ofisi za Serikali za mitaa na kamwe hawatashiriki vikao vya kamati ya maendeleo ya kata.
Walisema hawatajihusisha kusimamia suala la ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kuwafichua waovu katika maeneo yao kama ilivyokuwa awali.
“Sisi wenyeviti wa mitaa tunaelewa kwamba kitendo au hali ya kukabidhi au kutotumia mihuri kutasababisha athari kubwa katika mfumo wa uongozi na utoaji wa huduma kwa umma kwa ujumla.
“Athari hizo ni pamoja na wenyeviti wa mitaa na vijiji watashindwa kutoa huduma yoyote kwa wananchi kwa wakati na siku yoyote, hususan katika hati za dhamana mahakamani, vibali vya misiba, mikopo na barua za misamaha ya matibabu kwa wazee,” alisema Machicha na kuongeza:
“Mwongozo huu utasababisha mkwamo mkubwa wa utendaji wa Serikali za mitaa katika ngazi ya mitaa na kusababisha kuzagaa kwa silaha au uidhinishaji holela wa umiliki wa silaha hasa za moto.”
Pia alisema kuwa wananchi watatangatanga na kupata usumbufu mkubwa kwa kukosa huduma kwa wakati kutokana na ofisi za kata kuwa mbali kwa baadhi ya maeneo ya mitaa isiyo na watendaji.
Post a Comment