JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU KIKAO CHA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MHE.
PROF. SOSPETER MUHONGO (MB.) NA UJUMBE WA BENKI YA DUNIA KILICHOFANYIKA
TAREHE 28.09.2016
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu kikao cha
Waziri wa Nishati na Madini na Ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika
tarehe 28.09.2016 kikihusishwa na kupandishwa kwa bei ya umeme kama
ilivyoripotiwa na magazeti ya Mwananchi ya tarehe 12.01.2017 lenye
kichwa cha habari “Prof. Muhongo alivyoshiriki kupandisha bei ya umeme”
na la tarehe 13.01.2017 lenye kichwa cha habari “Prof. Muhongo awekwa
mtu kati”.
Wizara inapenda kuutaarifu Umma kuwa, imekuwa ikifanya vikao na wadau
mbalimbali wakiwemo Taasisi za Umma, Binafsi na Washirika wa Maendeleo
yakiwemo Mashirika ya Kifedha ya Kimataifa. Lengo la vikao hivyo ni
pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Nishati na Madini
nchini.
Aidha, tarehe 28/9/2016 Wizara ilifanya kikao na Ujumbe kutoka Benki ya
Dunia ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya majadiliano kuhusu upatikanaji wa
mkopo wa Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya kuboresha uendeshaji
wa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO). Kikao hicho pia kilihudhuriwa
na taasisi nyingine zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania
(TPDC), Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA).
Katika kikao hicho masuala yaliyojadiliwa yalikuwa ni;
1. Upatikanaji wa umeme wa kutosha, uhakika na bei nafuu kwa ajili ya
kuchochea shughuli za maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo
viwanda, biashara, kilimo na huduma za jamii;
2. Kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO); na
3. Kupunguza deni la TANESCO.
Katika kulipunguza deni la TANESCO ambalo linakaribia Shilingi Bilioni
800 (takriban Dola za Marekani Milioni 363) na kuboresha shughuli za
utendaji za TANESCO, Benki ya Dunia ilijadiliana na Serikali ya Tanzania
kupitia Wizara ya Nishati na Madini ili kupata mkopo wa Dola za
Marekani Milioni 200. Hivyo, katika kikao hicho, hakukuwa na makubaliano
ya kupandisha bei ya Umeme kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo.
Vile vile, tunaomba kuutaarifu Umma kwamba Wizara ya Nishati na Madini
kwa niaba ya Serikali inafanya majadiliano na Benki ya Maendeleo ya
Africa (AfDB), Umoja wa Ulaya (EU), JICA (Japan), na Mashirika mengine
ya fedha kwa lengo la kutafuta fedha za kuboresha Sekta ya Nishati.
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
13.01.2017
Post a Comment