Siku zote maisha ya binadamu yanaongozwa na uchaguzi tunaoufanya kila
siku. Uchaguzi huo ndio unatufanya tuwe na maisha haya au yale. Kama
uchaguzi unaoufanya ni mbovu kila siku, basi ni wazi na maisha yatakuwa
mabovu vilevile. Na kama uchaguzi wako ni mzuri, halikadharika na maisha
yako yatakuwa mazuri vivyo hivyo.
Kitu cha kuwa makini nacho hapa, angalia uchaguzi unaoufanya kila siku
na kila wakati. Uchaguzi huo ndio unaoamua maisha yako ya kesho yaweje.
Kama ni hivyo, ni lazima kwetu kufanya uchaguzi utakaotupa maisha bora.
Jaribu kujiuliza, ni uchaguzi wa mambo gani unaotakiwa kuufanya ili
kukupa mafanikio makubwa?
1. Chagua kutumia fursa vizuri.
Kwa fursa yoyote inayojitokeza mbele yako, jifunze kuitumia vizuri. Kama
ni fursa ya kibiashara au elimu itumie vizuri mpaka uone mafanikio
yake. Acha kucheza na fursa yoyote ya kimafanikio inayojitokeza mbele
yako. Ikiwa utafanya hivyo elewa ni lazima ipo siku utakuja kujuta kwa
uamuzi ulioufanya leo.
Kuna watu ambao wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokuwa makini na
fursa zilizojitokeza kwao. Bila shaka umeshawahi kuwaona watu hawa ambao
wana majuto na majonzi makubwa kila wakikumbuka ujinga walioufanya.
Hili ni tatizo linalosababisha ndoto za wengi kukwama. Ili ufanikiwe,
jifunze kutumia kila fursa vizuri.
2. Chagua kuishi na watu chanya.
Siku zote ukiwa mtu wa kuishi na watu hasi basi ni wazi utapata matokeo
wanayopata watu hao. Kama ni kulalamika, kulaumu ama kukosa mafanikio,
utapata matokeo kama hayohayo. Hakuna kikubwa utakachoweza
kukibadilisha. Mara nyingi maisha yetu yanathiriwa sana na wale watu
wanaotuzunguka.
Siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye watu wanaokuzunguka pia. Sio rahisi
kuishi na watu hasi, halafu ukategemea mafanikio, sahau hilo. Ni lazima
watakurudisha nyuma. Watu wenye mafanikio makubwa wanalijua hili. Hata
wewe ukitaka kufanikiwa chagua kuishi na watu chanya. Utajifunza mengi
huko na utafika mbali kimafanikio.
3. Chagua kufanya kazi kwa bidii.
Kitu kitakachokutoa hapo ulipo na kukufanikisha ni kufanya kazi kwa
bidii. Kazi yoyote unayoifanya jitoe kuifanya kwa nguvu zote mpaka
uifanikishe. Acha kufanya kazi kwa mkono mlegevu utajikwamisha kwenye
kwa mambo mengi kuliko unavyofikiri. Ile hali ya uvivu uliyonayo
jitahidi uitoe na kisha endelea kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii.
Watu wenye mafnikio makubwa siku zote wanafanya kazi kwa bidii na
kuhakikisha kuona mipango na malengo yao yanatimia. Kumbuka hakuna kitu
utakachokipoteza ikiwa utajitoa kwa moyo kufanya kazi zako kwa bidii.
Zaidi utajiongezea ujuzi, maarifa na uzoefu mkubwa utakaoutumia leo na
kesho kwa maisha yako.
4. Chagua kukabiliana na matatizo na kuyashinda.
Tatizo lolote unalokabiliana nalo unao uwezo wa kulishinda. Hakuna
tatizo lilokubwa kwako ambalo linaweza likakushinda. Kwa kulijua hilo
chukua jukumu la kuchagua kukabiliana na tatizo lako na acha kuruhusu
hata kidogo hilo tatizo likakushinda.
Tumia uwezo wako mkubwa wa akili uliopewa, tafakari kisha tafuta njia
sahihi za kuweza kukabilana na tatizo lako. Kwa kufanya hivyo utakuwa
mshindi na hakuna ambacho kitashindikana kwao. Wanamafanikio wote siku
zote huwa ni watu wakukabiliana na matatizo yao na siyo kuyakimbia.
5. Chagua kujifunza.
Ipo haja ya kutafuta mafanikio huku ukiwa unajifunza. Unapojifunza
inakusaidia kujua mambo mengi sana ambayo utayatumia katika safari yako
ya mafanikio. Huu ni uchaguzi muhimu sana kuufanya ili kujihakikishia
nafasi kubwa ya mafanikio katika maisha yako. Jifunze kupitia vitabu,
semina au warsha mbalimbali itakusaidia sana.
Hivi ndivyo ambavyo unaweza ukachagua mambo haya na yakawa nguzo na msaada mkubwa wa mafanikio siku zote.
Nikutakie ushindi katika safari yako ya mafanikio na kumbuka tupo pamoja.
Post a Comment