WINGA wa timu ya Simba, Shiza Kichuya, ameweka wazi kwamba ukame wake
wa mabao umekuja baada ya kugundua halikuwa jukumu lake kuhakikisha
anafunga katika kila mchezo, wakati wapo wachezaji wanaocheza nafasi
halisi zenye jukumu hilo.
Kichuya ambaye alijiunga na Simba msimu huu akitokea klabu ya Mtibwa
Sugar, alianza kwa kasi ndani ya klabu ya wekundu wa Msimbazi na Ligi
Kuu Tanzania Bara, baada ya kufumania nyavu mara tisa ndani ya michezo
13 pekee.
Mara ya mwisho winga huyu kufunga bao ilikuwa dhidi ya Stand United,
Novemba mwaka jana mjini Shinyanga, katika mchezo wa ligi ambao klabu ya
Simba iliibuka kidedea huku Kichuya akifunga bao hilo kwa mkwaju wa
penalti.
Shaffihdauda.co.tz imezungumza na Kichuya, ambapo amesema alikuwa
akijipa jukumu kubwa ambalo si lake na kusababisha kuwa mchoyo wa kutoa
pasi za mabao kwa wachezaji wenzake uwanjani.
“Kila mchezaji ana jukumu la kufunga na kuisaidia timu pale inapozidiwa
lakini wapo wachezaji ambao wanacheza nafasi zinazowafanya kuwa na
jukumu hilo la kupachika magoli kama vile Mavugo, Ajibu, Liuzio na
wengine,” – Kichuya.
“Simaanishi kwamba wachezaji wengine hawapaswi kufunga, lakini kuna wachezaji ambao wao jukumu lao ni kufunga mabao.”
Mchezaji huyo ambae kwasasa amekuwa akitokea benchi alisema Kwa sasa
hatolazimisha kufunga kama ilivyokuwa zamani: “Nitakuwa nikitoa pasi za
mabao zaidi labda niwe katika nafasi ya kufunga ndio nitafanya hivyo.”
Post a Comment