UPANDE wa utetezi katika kesi inayomkabili mfanyabiashara Ndama Hussein
maarufu kama Mtoto wa Ng’ombe, umeiomba mahakama kuliondoa shitaka la
kutakatisha Dola 540,390 za Marekani (Sh. bilioni 1.181) kwa madai hati
ya mashtaka ina mapungufu ya kisheria.
Utetezi unadai kwamba hati ya mashtaka dhidi ya Ndama ina mapungufu ya kisheria na kwamba wanaiomba mahakama kulifuta shtaka hilo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Leonard Challo, uliomba mahakama kutoa muda kwa ajili ya kujibu hoja za utetezi kuhusu kuliondoa shtaka hilo.
Katika kesi ya msingi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, alidai Februari 20, mwaka 2014, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na lengo la kudanganya alighushi nyaraka za kusafirisha madini.
Ilidaiwa alighushi nyaraka hizo akionyesha Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited imepewa kibali cha kusafirisha boksi nne za vipande wa dhahabu zenye uzito wa kilo 207 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 8.2 kwa Kampuni yenye makazi yake Australia inayojulikana kama Trade TJL DTYL Limited huku akijua ni za uongo.
Katika shtaka la pili, inadaiwa Machi 6, 2014, jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya kudanganya, aliandaa nyaraka za uongo kuonyesha kwamba hati ya kuondolea mizigo kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa za tarehe hiyo, akiwa na lengo la kuonyesha kwamba vipande vya dhahabu vyenye uzito wa kilo 207 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kuwa zinasafirishwa na Kampuni ya Muru Platinum kwenda Australia.
Katika shtaka la tatu, inadaiwa Februari 20, 2014 jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya alighushi nyaraka zikionyesha kuwa ni fomu ya tamko la kodi akionyesha Kampuni ya Muru Platinum imelipa Dola za Kimarekani 331,200 kama kodi ya kuingiza mzigo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kilo 207 ya vipande vya dhahabu vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 8,280,000 kutoka DRC huku akijua ni uongo.
Kwa mujibu wa shtaka la nne, Februari 20, 2014 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na nia ya kudanganya, alitengeneza nyaraka za uongo kuonyesha ni za bima kutoka Kampuni ya Phoenix Ltd za terehe hiyo, akilenga kuonyesha kwamba Kampuni ya Muru Platinum imekatia bima boksi nne za vipande vya dhahabu zenye uzito wa kilo 207 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 8,280,000 huku akijua ni uongo.
Katika shtaka la tano na sita, kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014 jijini Dar es Salaam, alijipatia kwa njia ya uongo na kutakatisha Dola za Kimarekani 540,390 (Sh. bilioni 1.181) kutoka Kampuni ya Trade TJL DTYL Limited kwa madai kuwa angesambaza na kusafirisha nje kilo 207 za vipande vya dhahabu vyenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000, lakini hakufanya hivyo.
Ilidaiwa mshtakiwa alitakatisha fedha hizo zilizopatikana kwa njia ya jinai kwa kuelekeza kiasi hicho cha fedha kuingizwa katika akaunti iliyopo benki ya Stanbic yenye jina la Kampuni ya Muru Platinum na baadaye alizitoa zote na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi huku akijua zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.
Mahakama itasikiliza hoja za Jamhuri Aprili 18, mwaka huu.
Post a Comment