Asante Kwasi
BEKI wa Simba, Asante Kwasi amewafanyia kitu mbaya timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza katika mchezo wa juzi uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, kufuatia kitendo cha kusikiliza maelekezo waliyokuwa wakipewa wachezaji wa timu hiyo na kocha wao, Ettiene Ndayiragije. Mara kadhaa Kwasi amekuwa akifanya kitendo hicho anapoona wachezaji wa timu pinzani wameitwa na kocha wao na kuanza kupewa maelekezo pindi mchezo unapokuwa umesimama.
Katika mchezo uliochezwa juzi Jumatatu kati ya Simba dhidi ya Mbao, Kwasi alikwenda katika benchi la Mbao zaidi ya mara tatu kusikiliza maagizo waliyokuwa wakipewa wachezaji wa timu hiyo kisha kwenda kuwaambia wenzake kinachojiri.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kwasi alisema kuwa, kitendo alichokuwa akikifanya ni mbinu ya kiuanamichezo kuweza kuwamaliza wapinzani wao kwa lengo la kufahamu maelekezo wanayopewa ili kuyafanyia kazi.
“Tumefurahi matokeo haya ya ushindi wa mabao matano, lengo letu ni kuona tunafanikiwa kufanya vizuri kila mechi tunayocheza ili tutwae ubingwa mwishoni mwa msimu huu.
“Mara nyingi nimekuwa nikienda kwa benchi la wapinzani kusikiliza, hii ni moja ya mbinu ya kimchezo ambayo inasaidia kuwasoma wapinzani wetu na kujua wanataka kufanya nini ili kuweza kujihami, ni mbinu ya kawaida ambayo inafanywa sehemu yoyote,” alisema Kwasi. Beki huyo aliyejiunga na Simba katikati mwa msimu huu akitokea Lipuli, paka sasa ana mabao sita katika Ligi Kuu Bara.
Post a Comment