0

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kukusanya na kutumia Sh1.21 trilioni katika mwaka wa fedha 2018/19, Makisio hayo ni makubwa yakilinganishwa na bajeti ya Sh1.08 trilioni ya mwaka huu.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed alitoa tathmini hiyo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar alipowasilisha mapendekezo ya mwelekeo wa uchumi na mpango wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha. Kati ya fedha hizo, alisema Sh787.2 bilioni zitatokana na vyanzo vya ndani, Sh387.7 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo na Sh35 bilioni mikopo.

Kuhusu matumizi, alisema Sh671.8 bilioni zitakuwa za matumizi ya kawaida wakati Sh508.5 bilioni zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo. “Kwa mwaka 2018/19 vipaumbele vya Serikali ni kuimarisha miundombinu ya usafiri hasa wa kuingia nchini, utalii, viwanda vidogo na kilimo kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji,” alisema.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo elimu, afya na upatikanaji wa majisafi na salama, kuendeleza utafiti, kukuza uwezo wa rasilimali watu, kuimarisha ajira kwa vijana na utawala bora.

Akitoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti iliyopo, Mohamed alisema katika nusu ya kwanza ya mwaka, tayari Sh463.8 bilioni zimetumika ambazo ni sawa na asilimia 77 ya makadirio katika kipindi hicho.

Kati ya kiasi kilichotumika, alisema Sh298 bilioni zilielekezwa kwenye matumizi ya kawaida, Sh165.5 bilioni kwenye miradi ya maendeleo Sh138.8 bilioni zikilipa mishahara ya watumishi wa umma.

“Mishahara imeongezeka kwa asilimia 39.6 kunatokana na kupandisha kima cha chini cha watumishi wa umma kutoka Sh150,000 hadi Sh300,000 kwa mwezi,” alisema.

Kwa miezi hiyo sita, alisema Serikali imekusanya Sh460 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 85 ya makadirio. Kati ya fedha hizo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) upande wa Zanzibar ilikusanya Sh126 bilioni ambazo ni asilimia 100 ya makadirio yaliyoongezeka kwa asilimia 24.7 wakati Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ikikusanya Sh161.9 bilioni sawa na asilimia 92.7, ongezeko la asilimia 27.9.

Post a Comment

 
Top