0

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kunakolifanya Taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na kimbilio la wale waliovurugikiwa na amani katika nchi zao.

Kadhalika, uwepo wa amani nchini si tu unatoa fursa ya kutekeleza majukumu ya kiuchumi na kijamii bila hofu bali pia ni sababu muhimu ya wenzetu wengine kutoka nje kuona fursa ya kuwekeza na kushirikiana nasi katika kujenga maendeleo ya nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 28, 2018) wakati akizindua Umoja wa Kimataifa wa  Wabunge Wapenda Amani tawi la Tanzania (IAPP), kwenye mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa Bungeni, jijini Dodoma.

Amesema amani na utulivu ni tunu kubwa sana katika jamii yoyote ile Duniani na Tanzania muda wote imeendelea kuenzi tunu hiyo iliyojengwa kwenye misingi imara kupitia waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Shirikisho la Amani kwa Wote  (Universal Peace Federation (UPF), ambalo lilianzishwa kwa lengo la kumkomboa binadamu kutoka katika udhalili wa kukosa mahitaji muhimu.

"Hili linadhihirika kupitia mipango ya shirikisho hilo ya kushirikiana na jamii nyingine katika kuimarisha sekta zenye kugusa maisha ya watu wengi kama vile kilimo, mazingira, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo," amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mipango hiyo utategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu katika jamii husika, ambapo amewahakikishia kwamba Serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana nao katika nyanja hizo za kijamii na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda maslahi ya pande zote mbili na kuwaletea maendeleo wananchi.

Post a Comment

 
Top