0
WAMILIKI wa nyumba katika Kata ya Kerege Wilayani hapa, wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na vyoo vinavyoeleweka na visafi ili kuepuka kupata magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu.

Wito huo kwa wenye nyumba ulitolewa juzi na Diwani wa Kerege, Said Ngatipura wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara ambao uliitishwa kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi.

Ngatipura alisema kuna baadhi ya nyumba hazina vyoo ambapo wapangaji waliopanga katika nyumba hizo hulazimika kwenda kujisitiri kwa majirani.

Alisema kuna nyumba nyingine zina vyoo, lakini havieleweki na ni vichafu hali ambayo ni mbaya kiafya kwa wanaovitumia kutokana na kwamba kupata magonjwa ya mlipuko ni rahisi kwao.

Ngatipura alisema kila mwenye nyumba ambaye anajua choo nyumbani kwake hakieleweki na ni kichafu ama hakipo kabisa ni heri kufanya marekebisho ya haraka kabla sheria haijachukua mkondo wake.

Alisema kuanzia sasa wataanza operesheni ya suala zima la usafi wa mazingira ambalo litaenda sambamba na ukaguzi wa vyoo kila nyumba.

"Wakati wowote kuanzia sasa tutaanza utaratibu wa kukagua usafi wa mazingira kila nyumba ambapo pia tutatumia nafasi hiyo kukagua na vyoo, hivyo mwenye nyumba ambaye anajuwa nyumbani kwake mazingira siyo mazuri na choo hakieleweki ama hakipo ni vema akafanya marekebisho haraka kabla hatujamfikia, " alisema Ngatipura.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa hawataangalia sura ya mtu au cheo chake.

Post a Comment

 
Top