Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema
kiwango kilichoonyeshwa na aliyekuwa kipa wao, Juma Kaseja ambaye kwa
sasa anaichezea Kagera Sugar, ni cha kawaida na kudai kuwa hajaona cha
ziada kwake.
Simba ilipoteza mchezo wake wa Jumapili dhidi ya Kagera Sugar na
kujikuta ikiwa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 55
nyuma ya Yanga yenye pointi 56, huku kipa Kaseja akionekana kuwa kikwazo
kutokana na umahiri ambao aliuonyesha uwanjani.
Hans Poppe alifunguka kuwa, kiwango kilichoonyeshwa na Kaseja katika
mechi dhidi ya Kagera ni cha kawaida kama alivyokuwa akicheza katika
timu yao na kudai kuwa hakuona cha ziada kutoka kwake.
“Ndiyo Kaseja alikuwa mchezaji wetu na aliondoka katika timu yetu miaka
kadhaa iliyopita, vilevile amecheza katika timu mbalimbali, kwa upande
wangu naona kiwango ambacho amekionyesha katika mechi dhidi ya Kagera ni
cha kawaida kama vilevile alivyokuwa akicheza alipokuwa Simba na
sijaona cha ziada kutoka kwake, anacheza kama ilivyo kwa makipa wengine.
“Wachezaji wengi wamekuwa wakiondoka na wanaonyesha viwango vya kawaida
lakini mwisho wa siku Simba inabakia kuwa ileile,” alisema Hans Poppe.
Post a Comment