Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke limeua watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema tukio hilo ni la Oktoba 21 baada
ya polisi kupata taarifa za kuwepo kwa kundi la watu wanaodhaniwa ni
majambazi.
Alisema
baada ya taarifa, kikosi kazi cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, kilifanya ufuatiliaji na kubaini nyumba ambayo haijakamilika
imezungushiwa uzio na muda wote mlango wa uzio huo ulikuwa umefungwa.
Aliongeza
kuwa uchunguzi wa kina, ulifanyika na kubaini kuwa kweli kundi hilo,
lipo ndani ya nyumba hiyo na kwamba muda mwingi mlango wa uzio, hufungwa
na kuongeza kuwa majira ya saa tano askari wa kikosi kazi cha mkoa huo
na mkoa wa Pwani, kilizingira nyumba hiyo.
“Baada
ya kujipanga mlango wa uzio huo uligongwa na kutoa amri ya kuwataka
walioko ndani ya nyumba hiyo wafungue mlango na kujisalimisha, lakini
tulishangaa baada ya amri hiyo ghafla milio ya risasi ilianza kutoka
ndani ya nyumba hiyo,” alisema Muroto.
Aliongeza
kuwa baada ya milio hiyo, askari ambao walikuwa makini na wakiwa
wamezingira nyumba hiyo wakiwa wamejipanga katika miundo ya mapigano,
walianza mashambulizi kujibu mashambulio hayo.
Alisema
majibizano yaliendelea na watu hao waliokuwa wanashambulia kutoka
ndani, walivunja uzio na watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya watano
walitoka huku wakiwa wanashambulia.
Muroto
alisema askari waliendelea kupambana nao na kufanikiwa kuwajeruhi
baadhi yao, na wengine walifanikiwa kutoroka na silaha zao.
“Mashambulizi
kutoka ndani yalitulia na askari waliingia ndani ya uzio, kwa kuwa
yalikuwa mapambano ya nguvu walikuta majambazi watatu wanaokadiriwa kuwa
na umri kati ya miaka 25 na 30 wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi na hali
zao zilikuwa mbaya na tuliwapeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini
walibainika kuwa tayari wameshakufa na miili yao imehifadhiwa hapo
ikisubiri kutambuliwa,” alisema.
Alisema
baada ya kufanya upekuzi, polisi walikuta silaha moja aina ya short gun
pump action yenye MV.51516 R na namba ya usajili TZ car 99987 na risasi
tano ndani ya magazini yake.
Risasi nyingine sita za short gun zilikutwa ndani ya mfuko wa plastiki pamoja na risasi nane za pistol.
Aidha
alisema katika tukio hili, ilibainika kuwa kuna askari mmoja
alijeruhiwa bega lake la kushoto na lilikuwa jeraha kubwa la risasi,
hivyo alipelekwa katika Hospitali ya Muhimbili ambako amelazwa na
anaendelea kupata matibabu akisubiri kufanyiwa upasuaji.
Muroto
alisema ufuatiliaji wa majambazi, walitoroka eneo la mapambano
uliendelea kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mtambani, ambapo
majira ya saa tatu asubuhi jambazi mmoja alipatikana akiwa mahututi na
juhudi za kumfikisha hospitali zilifanyika. Hata hivyo, alikufa akiwa
njiani.
”Tunawashukuru
wananchi wote wema kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa Jeshi la
Polisi, kwa kuliunga mkono katika kufichua wahalifu na kupambana na
wahalifu, nitoe tahadhari kuwa mkoa huu ukifanya tukio ujue
utashughulikiwa kabla hujakamilisha na ukifanikiwa kukamilisha azma yako
haitachukua muda utakamatwa,” alisisitiza.
Post a Comment