MAKAMU
wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameelezea kukerwa na vitendo vya rushwa na
kuwataka wanawake wajasiriamali kufichua kila aina ya rushwa
wanazoombwa na wenye mamlaka katika sekta ya biashara nchini.
Alisema
hayo jana wakati akifungua kongamano la wajasiriamali wanawake
lililoandaliwa na Mtandao wa Sauti ya Wajasiriamali Wanawake Tanzania
(VOWET) na kuhudhuriwa na wanawake zaidi ya 500.
Alisema
iwapo wanawake wakiwafichua waombaji wa rushwa wanaokwamisha harakati
zao za kusonga mbele kibiashara, itaiwezesha serikali kuondoa kero hiyo.
Samia
alisema baadhi ya wanawake wanaombwa rushwa za ngono na nyinginezo na
hukaa kimya bila ya kulifikisha suala lao hilo kwa mamlaka husika ili
wasaidiwe na kwamba kukaa kimya kumechangia kuendelea kuwepo kwa kero
hiyo.
Amewahakikishia
wanawake hao kuwa serikali itakuwa ikiwapa kipaumbele kwenye malipo ya
fedha za zabuni ili waweze kusonga mbele zaidi na kuongeza kuwa wapo
wanawake ambao wamekuwa wakijikita zaidi kwenye biashara, lakini
wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwamo hiyo ya kucheleweshewa fedha
zao.
Akizungumzia
kuwaunganisha wanawake na masoko, alisema ofisi yake inashughulikia
kutengeneza mtandao utakaotangaza kazi zote za wajasiriamali wanawake
kirahisi zaidi.
Alisema
wapo wajasiriamali wa nje ya nchi, lakini wakitaka kufahamu fursa za
biashara zinazofanywa na wanawake wanashindwa kupata taarifa zao na
kuwahakikishia kuwa ofisi yake inalitatua tatizo hilo.
Rais
wa Vowet, Maida Waziri katika hotuba yake alimueleza Makamu wa Rais
kuwa malipo ya kodi kwa makadirio ya nyuma yanakwamisha maendeleo ya
wanawake nchini.
Alimuomba
Makamu wa Rais kuwasaidia kufutwa kwa mfumo huo kwa kuwa licha ya
kuwaathiri wajasiriamali kiujumla ila wanawake wanaathirika zaidi kwa
kuwa wanalipa fedha ambazo hawana taarifa nazo.
Post a Comment