Wakati
Mfalme wa Morocco, Mohamed VI akitarajiwa kuwasili leo nchini kwa ziara
ya kikazi, huenda akapokewa kwa mabango baada ya vijana wanaounda
kamati ya mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC) kujipanga
kufanya hivyo kushinikiza nchi hiyo kuacha kuitawala kwa mabavu Sahara
Magharibi.
Vijana
hao wamefikia uamuzi huo kutokana na kile walichodai kusikitishwa kwao
na kitendo cha Morocco kuendelea kuitawala kwa mabavu nchi ya Sahara
Magharibi na kupuuza wito wa Umoja wa Mataifa (UN) unaoitaka kuipa uhuru
nchi hiyo.
Hata
hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia msemaji wake, Hassan Abass imesema
ujio huo ni muhimu kwa uhusiano wa kidiplomasia na uchumi.
“Serikali
ilishaeleza msimamo wake, kuna uhusiano wa aina nyingi, ujio huu ni
muhimu kwa uhusiano wa kidemokrasia na uchumi kama hisia zitawatuma
kufanya hivyo, wanapaswa kufuata sheria,” alisema Abass.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa TASSC,
Alphonce Lusako alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili
Morocco iiache huru Sahara Magharibi lakini watawala wa nchi hiyo
wamekuwa wagumu kuruhusu hilo.
Lusako
alieleza kuwa TASSC inafahamu fika kwamba Mfalme Mohamed VI amekuwa
akifanya ziara katika mataifa mbalimbali akijaribu kutafuta kuungwa
mkono ili Morocco iendelee kuitawala Sahara Magharibi.
Alisema
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoitambua Sahara Magharibi
inapaswa kumuonyesha wazi Mfalme Mohamed VI kuwa haiungi mkono utawala
wa kimabavu.
“Tunamtaka
Mfalme wa Morocco kuacha mara moja vitendo vya kibeberu vya kuikalia
Sahara Magharibi sambamba na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na
wanaharakati wanaoshikiliwa magerezani katika maeneo yanayokaliwa
kimabavu.
"Ni
aibu kwa nchi moja ya Kiafrika kuitawala nchi nyingine: Tunaunga mkono
msimamo wa Tanzania wa kuendelea kuitambua na kuiunga mkono Sahara
Magharibi kwenye vyombo vya kimataifa na tunasisitiza isiyumbishwe
katika msimamo huo, ” alisema.
Katibu
wa TASSC, Jasper Hassan alisema tangu kamati hiyo ianzishwe mwaka jana
imekuwa ikifanya harakati mbalimbali ikiwamo mihadhara ya wazi
inayolenga kuisukuma Morocco kuacha kuitawala Sahara Magharibi.
“Jitihada
zilianza muda mrefu ila mwaka jana ndiyo vijana tukaona tuingilie kati
tukiwa kama Waafrika, tunapinga kila aina ya unyonyaji tunataka Sahara
Magharibi iwe huru,” alisema Hassan.
Juzi,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ziara ya kiongozi
huyo itakuwa na manufaa kwa nchi, kwani akiwa na mwenyeji wake, Rais
John Magufuli watasaini makubaliano 11 ya ushirikiano katika sekta za
kilimo, gesi, mafuta, Reli ya Liganga na Mchuchuma na sekta ya utalii.
Post a Comment