0
Mfanyakazi wa ndani wa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Angella Kizigha, Miraji Mkanga (41) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa madai ya kumwibia mwajiri wake vitu ikiwemo bastola yenye risasi 23, simu, mikufu na bangili za dhahabu, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 85.

Akisomewa mashitaka hayo na Karani Dayz Makalala mbele ya Hakimu Joyce Mushi, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Mkanga alitenda kosa hilo Oktoba 2, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Makakala alidai mtuhumiwa huyo aliiba Dola za Marekani 3,500 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 7.5, bangili za dhahabu gramu 300 zenye thamani ya Sh milioni 36, hereni gramu 450 zenye thamani ya Sh milioni 42, doti 30 za vitenge zenye thamani ya Sh milioni 1.5 na shuka 10 zenye thamani ya Sh 700,000.

Aidha, mfanyakazi huyo wa ndani anatuhumiwa kuiba bastola moja iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech yenye namba No B 283994 na risasi 23 thamani ya Sh milioni mbili, simu mbili za Samsung zenye thamani ya Sh 500,000 na nguo tofauti zenye thamani ya Sh 750,000 mali ya mbunge huyo ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mshitakiwa alikana shitaka hilo wakati huo dhamana yake ipo wazi, akitakiwa kuwa na wadhamini wawili kutoka katika taasisi inayotambulika na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Novemba 28, mwaka huu, na mshitakiwa alirudishwa rumande kutokana na wadhamini wake kutofika huku upelelezi ukiendelea.

Post a Comment

 
Top