0
BEIJING, China
KATIKA miaka ya hivi karibuni, Ligi Kuu nchini China imeonekana kuwa tishio kwa zile za barani Ulaya, zikiwamo Ligi Kuu England na La Liga, ambazo awali zilionekana kuwavuta mastaa wengi.
Klabu mbalimbali za China zimeonyesha jeuri ya fedha kwa kushindana na soka la Ulaya na kwa kiasi kikubwa zimefanikiwa kusajili wachezaji wenye majina makubwa.
Kwa upande mwingine, kufuru ya fedha ya klabu za China imeonekana kuwa mwiba mchungu kwa makocha wa Ulaya, akiwamo Arsene Wenger.
Mpaka sasa straika anayemtegemea, Alexis Sanchez, amegoma kusaini mkataba mpya wa kubaki klabuni hapo.
Wakati mvutano huo ukiendelea, ambapo chanzo chake ni Sanchez kutaka ongezeko la mshahara, kuna klabu moja ya China imetangaza kumlipa mshahara mnono staa huyo wa kimataifa wa Chile.
Bado jina la klabu hiyo halijawekwa wazi, lakini taarifa zisizo na shaka zimethibitisha kwamba, iko tayari kumsajili Sanchez na kumpa kiasi cha pauni 300,000 kwa wiki.
Hilo limeanza kumuumiza kichwa Wenger, kwani haonekani kuwa na ujasiri wa kumlipa nyota huyo kiasi hicho cha fedha.
Lakini pia, matajiri wa Shanghai Shenhua wanataka kumnasa straika wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez, ambapo imeelezwa kuwa mshahara wake utakuwa wa kufa mtu.
Taarifa zilizopo zimenyetisha kuwa, wakali hao wanataka kumfanya Tevez kuwa mmoja kati ya wanasoka wanaolipwa fedha nyingi kwa kumpa mshahara wa pauni 615,000 kwa wiki.
Oscar wa Chelsea naye anatajwa kuwa mbioni kutua China, ambapo imeelezwa kuwa, atajiunga na kocha wake wa zamani, Andre Villas-Boas, katika kikosi cha Shanghai SIPG.
Wachina watatumia pauni milioni 52 kumsajili na mshahara wake utakuwa pauni 400,000 kwa wiki.
Cha kushangaza zaidi ni tetesi zilizoibuka hivi karibuni zikidai kuwa Hebei China Fortune wanamtaka Lionel Messi na watamlipa pauni milioni 80 kwa mwaka.
Inaaminika kuwa, huenda uwepo wa Muargentina mwenzake, Lavezzi, kwenye kikosi hicho ukamshawishi Messi kufumba macho na kutua China.
Wakati Graziano Pelle alipotua Shandong kwa ada ya pauni milioni 13 akitokea Southampton, alishika nafasi ya tano kwenye orodha ya mastaa wanaolipwa fedha nyingi duniani.
Pelle alikuwa akikunja kitita cha pauni milioni 13.5 kwa mwaka.
Mpaka sasa, mastaa kibao wameshatekwa na fedha za Wachina, wakiwamo Alex Teixeira, Ezequiel Lavezzi, Ramires, Papiss Cisse, Gervinho, Asamoah Gyan, Pelle na Demba Ba,
Teixeira akiwa na umri wa miaka 26, alijiunga na Jiangsu Suning kwa ada ya pauni milioni 38, huku Ramires akimfuata kwa dau la pauni milioni 25.
Kuna kipindi Hulk alikuwa akipokea pauni 340,000 kutoka kwa mabosi wake wa Shanghai SIPG na kuwa mchezaji wa tatu kupokea mshara mnono duniani nyuma ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Januari mwaka huu, klabu za China zilitumia pauni milioni 208 katika dirisha dogo la usajili. Kwa kufanya hivyo, zilizifunika zile za Ligi Kuu England.
Wakati saini yake ikifukuziwa na klabu nyingi za Ulaya, staa wa zamani wa Arsenal, Gervinho, aliikacha klabu yake ya Roma na kujiunga na Hebei China Fortune.
Mkongwe wa Chelsea na timu ya Taifa ya Australia, Tim Cahill, alitimka Chelsea na kutua Hangzhou Greentown.
Baada ya kutesa na QPR na Sevilla, Stephane M’bia naye hakutaka kupitwa na mkwanja wa Wachina na ndipo alipokubali ofa ya kujiunga na Hebei China Fortune, akitokea Trabzonspor ya Uturuki.
Asamoah Gyan alikuwa na uwezo wa kusajiliwa na klabu kubwa za Ulaya na saini yake ilikuwa ikiwindwa vikali barani humo, lakini alitua Shanghai SIPG ambapo mkataba wake wa kwanza tu ulikuwa ukimpa pauni 225,000 kwa wiki.
Mastaa Wayne Rooney na John Terry wamekuwa wakihusishwa mara kadhaa na mpango wa kusajiliwa na timu za China. Huenda hayo yakatimia siku moja.

Post a Comment

 
Top