MKAZI wa kijiji cha Sakalilo, Laela mkoani Rukwa, Calistus Jacob
(44), ameuawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali kichwani na
kisogoni kisha kutupwa chini ya daraja la Mto Mumba na watu
wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Geoge Kyando, alisema juzi kuwa chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana na juhudi za Jeshi la Polisi zinaendelea ili kubaini.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alifika eneo la tukio na kujionea uhalisia wa jambo hilo na baadaye waliubeba mwili huo hadi hospitalini na kufanyiwa uchunguzi, hivyo kubainika kuwa aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kisogoni, kisha kutupwa mtoni.
Alisema mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kugundua kuwa alichomwa na kitu chenye ncha kali na kutupwa mtoni.
Kyando alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na tukio hilo na kwamba uchunguzi wa kipolisi unaendelea.
Aidha, Kamanda Kyando alisema atalifuatilia suala hilo na kuhakikisha anawakamata na kuwafikisha mahali husika wahusika wa tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Post a Comment