0
HIVI sasa kampuni zinazotengeneza magari na hasa ya kutumia dizeli, nyingi zinakabiliwa na mtihani kama magari yao ni salama kimiundombinu na mazingira.

Wakati Volkswagen ya Ujerumani sasa inakabiliwa na majanga ya kulipa faini ya mabilioni ya fedha kwa thamani ya dola za Marekani, Renault ya Ufaransa na Fiat ya Italia, nazo sasa zinachunguzwa.

Mwaka jana, kampuni hiyo ilikiri kuweka vifaa ‘feki’ na kuamriwa kulipa fidia ya Dola za Marekani bilioni 15(Sh. Trilion 32.7) kwa mamia ya magari yaliyouzwa nchini humo, ambayo yanatumia dizeli na kampuni hiyo imekubali kulipa fidia.

Nchini Hispania nako mwezi Oktoba, mwaka jana, mahakama iliamuru kwamba, wamiliki wa magari ya Volswagen kuwalipa wanunuzi kila mmoja, Paundi za Uingereza 4,300, katika nchi hiyo ambayo nayo ni soko kubwa.

Ni sakata linaloikabili kampuni ya Volkswagen, na wakati huohuo, umeziponza nchi za Ujerumani ambako ni makao makuu ya magari yanakoundwa na Uingereza, wakishambuliwa na Jumuia ya Ulaya (EU) kwa madai wameshindwa kuwachukulia hatua wazalishaji wa magari hayo, kwa makosa tajwa. Hatua ya kuwachukulia iko njiani.

Jumla ya magari ya dizeli yaliyouzwa na sasa yanakabiliwa na kashfa hiyo, inafikia milioni 1.2 duniani kote na iwapo watalipwa fidia wahusika, wanaweza kulipa wastani wa Paundi za Uingereza bilioni nne.

WAFANYAKAZI WAPUNGUZWA
Kufuatia madai yalitolewa na uamuzi dhidi ya Volkswagen, sasa kampuni hiyo inalazimika kuwaondoa kazini watumishi 30,000, hatua ambayo inatarajiwa isaidie kuokoa wastani wa Dola za Marekani bilioni 3.7 (Sh Trilioni.8.2)) kila mwaka, ambazo zitatumika kulipa fidia. Faini wanayodaiwa hadi sasa ni wastani wa dola za Marekani bilioni 15.

Ni uamuzi uliofikiwa, baada ya mvutano mkali kutoka kwa Chama cha Wafanyakazi, kuhusu upunguzwaji wa watumishi hao.

Hata hivyo, Pamoja na hatua hiyo ya kupunguza wafanyakazi wake, kampuni inajigamba kwamba iko kwenye mpango wa kuanza kuzalisha magari ya teknolojia inayotumia umeme, hatua inayotarajiwa kuzalisha ajira mpya 9,000.

Mtendaji Mkuu, Matthias Müller, anafafanua: “Ni ubunifu mkubwa wa maboresho, ambao hayajawahi kutokea katika historia ya kampuni.”

Kwa mujibu wa Muller, kampuni hiyo hivi sasa ina matawi 31 katika nchi mbalimbali na imeajiri wafanyakazi 600,000.

Wafanyakazi watakaopunguzwa ni wastani wa asilimia tano ya watumishi wote.

Kiongozi mwingine wa kampuni hiyo, Herbert Diess, anafafanua: “Wazalishaji wote wanapaswa kujijenga wenyewe, kwa kuwa Msukosuko umetuweka imara.”

Anadai kuwa, hadi sasa kampuni haijatetereka sana sokoni, hasa katika nchi za Ujerumani, Italia na Ufaransa ambako mauzo ya magari yameongezeka kwa asilimia kati ya tisa na 17.

MASHITAKA UINGEREZA

Kampuni ya Sheria ya Harcus ya Uingereza kwa niaba ya wateja 10,000 wa nchini humo, imefungua shauri la madai likitaka kila mteja alipwe wastani wa Dola za Marekani 3,000(zaidi sh. Milioni 6.5) ambakpo jumla ya madai ya wateja wote inafika Sh. Trilioni 6.5.

Katika dai hilo la kisheria mahakamani, wanadai walipotoshwa kuhusu namna magari hayo yanavyotoa mvuke wa moshi.

"Tunachoamua kukifanya hapa, ni kuhakikisha kwamba kama Volkswagen watapatikana na hatia ya kuwapotosha watumiaji kuhusu namna magari yao yanavyochafua mazingira, waadhibiwe inavyostahili ili kudhibiti tabia ya aina hii isitokee tena,” anasema mwanasheria Harcus Sinclair.

Mary Creagh, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira wa Bunge la Uingereza, anasema:"Serikali isipoingilia kati, wenye magari watajichukulia madaraka na kufanya wanavyotaka,kupitia maamuzi ya kimahakama."

MABOSI VW WATUHUMIWA

Kurugenzi wa masuala ya kisheria ya Marekani inawatuhumu mabosi sita wa kampuni ya Volkswagen,na inanuia kuwachukulia hatua dhidi ya kashfa hiyo. kati yao watano wako Ujerumani na mmoja Marekani.

Wahusika wanatuhumiwa kufanya njama kwa zaidi ya muongo mmoja, kuuza magari hayo yenye hitilafu katika usalama wa mazingira

“Watu hawa, wameshikilia nyadhifa tofauti na kuwajibika ndani ya Volkswagen (nchini Marekani), ikiwemo kusimamia maendeleo yake na kutumikia bodi ya kampuni,” unaeleza waraka mmojawapo wa kisheria.

Kampuni ya Volkswagen inatarajia kuwa chini ya msimamizi huru kwa miaka mitatu, akifuatilia ubora wa magari inayozalisha.

Aina ya gari la Volkswagen lililothibitika kukutwa na kashfa, inadaiwa kutoa moshi mara 40 zaidi ya ilivyoruhusiwa na mamlaka za Mazingira na viwango vya Marekani.

Mabosi wa kampuni hizo walikiri walipohojiwa mwaka 2006 kuhusu usahihi wa vifaa vya kudhibiti moshi, baada ya kugundulika wamepotosha kuhusu injini za gari.

Pamoja na kukiri, kwa ahadi ya kufanya ubunifu kwa kuiga teknolojia kutoka kampuni moja ya kimarekani, ili kukidhi viwango vya Marekani, bado walidaiwa kupotosha tena.

KASHFA DHIDI YA
RENAULT NA FIAT

Kampuni ya Renault kutoka Ufaransa, nayo haiko salama kama ilivyo kwa Volkswagen, kuhusu kupotosha ukweli wa mvuke utolewao katika mfumo wa injini yake ya dizeli.

Katika utetezi wake, inadai kwamba injini za magari yake ziko vizuri na zinaendana na viwango vya Ulaya, ikiwemo Ufaransa.

“Magari ya Renault siku zote yanaendana na sheria za Ulaya na viwango vyake. Hayajaundwa na vifaa vya udanganyifu ambavyo vinaathiri mifumo ya hewa chafu,” inajitetea katika taarifa yake.

Timu huru ya wachunguzi kutoka Ufaransa juu ya magari ya Volkswagen, ndio iliyoibua kashfa nyingine kwenye gari za Renault.

Inasema yanatoa moshi mwingi na kuhatarisha afya ya umma. Kwa mujibu wa wanasheria wa nchi hiyo, nao wanadaiwa kudanganya kama wenzao wa Volkswagen.

Tayari inadaiwa thamani ya kashfa hiyo imeshusha thamani ya hisa za kampuni hiyo kwa asilimia tatu.

Wakatai uchunguzi ukielekezwa kwa kampuni hiyo, watengeneza wengine wa magari kutoka Italia - Fiat nao wamekumbwa na dai kama hilo huko Marekani, kuhusu magari yao ya dizeli kwa kifaa cha kudhibiti na kutoa moshi wa ziada.

Fiat imekana madai hayo na imeomba kuundwa kwa tume huru ya kuichunguza.

Sakata la Volkswagen, liligunduliwa katika maabara ya mitambo na mhandisi Mmarekani, aliyewahi kufanya kazi na kampuni hiyo kwa muda mrefu.

Kutokana na kashfa hiyo, Uingereza imeiomba Marekani kuitumia taarifa za uchafuzi wa mazingira inayohusu magari ya Fiat Chrysler, ili nayo ianze ufuatiliaji.

Wakala wa Kutunza Mazingira wa Marekani, ilisema kati ya mwaka 2014 na 2016, waligundua baadhi ya matoleo ya magari ya Kimarekani aina ya Grand Cherokees na Dodge Ram 1500, yanatoa moshi wa ziada kuliko inavyotakiwa, kulingana na kiwango walichowekewa.

Post a Comment

 
Top