Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kujenga maduka ya kisasa zaidi ya 200 katika eneo lililobomolewa jengo la Billicanas lililokuwa likimilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Jengo la Billicanas lilibomolewa na shirika hilo mwishoni mwa wiki baada Mbowe kuondolewa mwanzoni mwa Septemba mwaka jana kutokana na kushindwa kulipa deni la Sh bilioni 1.3 ambazo zilikuwa pango ya miaka 20.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema ujenzi wa maduka hayo madogo madogo ya kisasa yatakayokuwa katika ghorofa tano, unatarajia kuanza mwakani baada ya kukamilika kwa taratibu za kutafuta mzabuni.
“Tunajenga mall (maduka ya kisasa) ndogo ndogo, maduka yatakuwa 232 yatakayoanzia ghorofa moja mpaka tano,” alisema Mchechu.
Alisema kabla ya kufanyika kwa ujenzi huo, wataalamu wa shirika hilo watapitia michoro iliyoandaliwa na baadae kutangaza tenda ili kupata mzabuni.
Mchechu alisema kuwa mbali ya jengo la Billicanas, kuna majengo mengine manne yanayomilikiwa na shirika hilo yatabomolewa ili kukamilisha ujenzi huo.
“Kuna majengo yanayozunguka eneo la maegesho ya magari ya jiji, tunategemea kuyabomoa kati ya majengo matatu au manne ndani ya mwezi huu, hilo litakuwa eneo la maegesho,” alisema Mchechu.
Alisisitiza kuwa ubomoaji wa majengo hayo utafanyika ndani ya mwezi huu ili kuweza kuharakisha ujenzi huo.
Post a Comment