0
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Estomihn Chang’a amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Frank Bahati kumsimamisha kazi mara moja afisa uvuvi msaidizi wa kata ya Bwiro Judith Msusa kwa tuhuma za kushirikiana na baadhi ya wavuvi wa kisiwa hicho kuisaliti serikali katika vita dhidi ya uvuvi haramu.

Agizo hilo limekuja siku moja baada ya mkuu huyo wa wilaya ya Ukerewe kushiriki katika zoezi la kuteketeza zana haramu za uvuvi zipatazo 1,250 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 190.3 zilizokamatwa na maofisa uvuvi katika kisiwa cha ukara wilayani humo wakati wa doria.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Frank Bahati akiwa katika ziara ya kukutana na wavuvi zaidi ya 200 wa kisiwa cha Bwiro, alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wavuvi hao wakimtuhumu afisa uvuvi msaidizi wa kata hiyo Bi. Judith Msusa kwamba amekuwa akikamata zana haramu za uvuvi na kisha kuziachia.

Afisa maendeleo ya jamii msaidizi tarafa ya Ukara Fortunata Salvatory amesema zoezi la kutokomeza uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe bado linakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kukosekana kwa boti ya serikali ya kufanyia doria hali inayowalazimu maafisa uvuvi wa tarafa hiyo kuomba boti kwa wavuvi pamoja na kutokuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa baadhi ya viongozi na watendaji.

Post a Comment

 
Top