0


Maafisa wa Emirates hawajafafanua iwapo nyoka aliyegunduliwa ana sumu

Safari ya ndege ya shirika la Emirates ya kutoka Oman kwenda Dubai imesitishwa baada ya wahudumu wa ndege kumpata nyoka ndani ya ndege.

Safari ya ndege nambari EK0863 kutoka Muscat ilisitishwa baada ya wafanyakazi wa kupakia mizigo kumgundua nyoka kwenye eneo la kubebea mizigo.

Msemaji wa shirika hilo la ndege amenukuliwa na vyombo vya habari Dubai akisema nyoka huyo aligunduliwa kabla ya abiria kuabiri ndege hiyo.

Ndege hiyo ilichunguzwa kwa makini kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.

Iliwasili Dubai saa chache baadaye.

Emirates hawakusema ni nyoka wa aina gani aliyepatikana kwenye ndege au iwapo ni nyoka hatari.

Wengi wamefananisha kisa hicho na filamu ya Samuel L Jackson ya mwaka 2006 kwa jina Snakes on a Plane (Nyoka kwenye Ndege) ambapo abiria wanakumbana na mamia ya nyoka wadogo wenye sumu ndege ikiwa katikati ya safari. Baadhi ya watu wameanza kujadili filamu hiyo mitandao ya kijamii.

Hii si mara ya kwanza kwa nyoka kugunduliwa kwenye ndege, hasa maeneo yenye joto.

Novemba mwaka jana, nyoka wa urefu wa mita tatu aligunduliwa kwenye ndege Mexico.

Chatu mwingine alionekana akining'inia kwenye ubawa wa ndege iliyokuwa safarini kutoka Cairns, Australia hadi Port Moresby nchini Papua New Guinea mwaka 2013.

Na mwaka 2012, maafisa wa kuwahudumia wanyama walimuokoa nyoka mdogo aliyegunduliwa kwenye ndege iliyowasili Scotland kutoka Mexico.

Post a Comment

 
Top