Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapindusi Zanzibar (SMZ), Dk. Khalid Salum Mohamed
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM ) umekataa kuhusishwa na shutuma dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapindusi Zanzibar (SMZ), Dk. Khalid Salum Mohamed kwa kuwa haina ushahidi wa moja kwa moja.
Pia, umesema utafanya kila linalowezekana kujua kama kweli madai yaliyotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis yana ukweli au ni mambo binafsi.
Juzi Sadifa alinukuliwa akisema waziri huyo amewahi kuwakataza vijana wa CCM kuvaa sare za chama hicho katika sherehe za Serikali.
Sadifa alisema kutokana na matamshi hayo waziri huyo ni mtu asiyetambua uzito wala thamani ya CCM na hatoshi kubeba dhamana aliyonayo.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Unguja jana na Kaimu Katibu wa Idara ya Hamasa, Sera, Utafiti na Mawasiliano Makao Makuu UVCCM, Mtemi Yaredi.
Alisema Kamati ya Utekekezaji ya umoja huo itakutana kujadili suala hilo na kulitolea ufafanuzi.
Mtemi Yaredi alisema matamshi ya mwenyekiti wao ni mazito hivyo kunahitajika upembuzi, ukusanyaji vielelezo na ushahidi ili UVCCM ijiridhishe na kujiweka katika mazingira salama.
“Kauli ya mwenyekiti au katibu mkuu hubeba sura ya jumuia kulingana na dhamana zao za kanuni na katiba.
“Hadi sasa hatuna ushahidi wa dai hilo, itaeleweka baadaye kama lina ukweli au ni msigano binafsi wa uhusiano,” alisema Yaredi.
Yaredi alisisitiza kuwa tuhuma hizo zimetamkwa na mtu mwenye dhamana kwa jumuia yao, litahesabiwa ni la UVCCM kwa wakati huu, lakini uhalisia hadi linatamkwa katika mkutano wa umoja huo ulikuwa haufahamu chochote.
“Tupo hapa Zanzibar karibu viongozi wote wa juu, Mwenyekiti Sadifa, Makamu Mwenyekiti Mboni Mhita, Kaimu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka, Naibu Katibu UVCCM Zanzibar, Abdulghafar Idrisa Juma na watendaji wa sekreterieti ya jumuiya, tunaomba muda wa kutafakari,” alisema.
Alipoulizwa kama aliyoyasema Sadifa hayatokani na hotuba ya maandishi aliyokuwa akiisoma, Mtemi Yaredi alisema hakukuwa na hotuba iliyoandikwa ikihusisha madai ya waziri kuwatimua vijana wa chama wasivae sare za CCM katika hafla za serikali.
Post a Comment