WATUMISHI
10 wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Mbeya (Ifisi) waliotimuliwa kazi na
Bodi ya hospitali hiyo kwa maelezo kuwa hawana sifa, wamezua sokomoko
hospitalini hapo baada ya kuorodhesha majina ya zaidi ya watumishi 20
wakidai walinunua vyeti.
Watumishi hao walifikisha orodha hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos
Makalla, wakidai kuwa watumishi hao walifanyiwa mpango na baadhi ya
viongozi wa hospitali hiyo kuwasaidia kununua vyeti hivyo.
Kwa mujibu wa watumishi hao, vyeti hivyo vilikuwa vinanunuliwa kwa Sh.
200,000 kutoka katika moja ya chuo cha uuguzi jijini hapa.
Mmoja wa watumishi hao walioondolewa hospitalini hapo, Subira Mwanjali,
alithibitisha kwenye mkutano kati ya Mkuu wa Mkoa na viongozi wa Kanisa
la Uinjilisti ambao ni wabia wa hospitali hiyo, kuwa yeye ni miongoni
mwa walioombwa fedha hizo kwa ajili ya kununuliwa cheti.
“Mimi ni miongoni mwa watu tulioambiwa tutoe Sh. 200,000 ili
nikanunuliwe cheti, lakini nilikataa kwa sababu ninacho cheti changu
halisi cha taaluma ya uuguzi. Walituondoa sisi na wakiwaacha watu ambao
tunaamini hawana vyeti ila wamenunuliwa,” alidai Mwanjali.
Naye Anne Mwangindwa, alidai kuwa uongozi wa hospitali hiyo uliwaondoa
kazini bila kufuata taratibu za kazi ikiwamo kutowalipa stahiki zao.
Alidai kwamba baada ya kuona hawatendewi haki, waliamua kupeleka
malalamiko yao kwenye Chama cha Wafanyakazi wa Afya nchini (Tughe) ili
wapate haki zao, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
“Sisi hatukatai kupunguzwa kazini, lakini tunachotaka ni kulipwa stahiki
zetu kama zinavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria za kazi, wamekuwa
wakituzungusha hivyo hatuna imani na hawa watu japo ni watu wa Kanisa,”
alisema Mwangindwa.
Kwa upande wake, Esther Mwaswalwiba, ambaye yupo upande wa kundi la
waliopunguzwa mishahara, alidai kuwa wamepunguzwa mishahara kutoka Sh.
320,000 mpaka 50,000, kiasi alichosema hakiwezi kuwasaidia kuendesha
maisha yao.
Alisema kupunguza mishahara hiyo ni sehemu ya kutaka kuwatengenezea mazingira ya kufukuzwa kabisa kama wenzao walioondolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Mchungaji Tito Nduka,
alikataa tuhuma zilizoelekezwa kwa uongozi wa hospitali hiyo kwa maelezo
kuwa watumishi hao wameondolewa kutokana na agizo la Rais la kuwaondoa
kazini watumishi wasio na vyeti.
Alisema watumishi hao waliondolewa na Bodi ya hospitali hiyo baada ya
kubainika kuwa hawana vyeti vya kidato cha nne na hivyo hakuna uonevu
wowote uliofanyika.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Makalla,
aliunda timu ya watu wanane kuchunguza mambo makuu matatu yaliyotajwa
kwenye malalamiko hayo.
Timu hiyo inaundwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina,
Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa
Mbeya, Xavery Mhywela, Maofisa Usalama wa Taifa, Katibu Tawala wa Wilaya
ya Mbeya na baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema kuwa timu hiyo itafanya kazi ndani ya siku 10 na majibu
yatakayofanya hatma ya watumishi hao ijulikane pamoja na waliotuhumiwa
kuhusika.
Alikabidhi timu hiyo baadhi ya nyaraka ambazo watazitumia kwenye
uchunguzi ikiwa ni pamoja na orodha ya watumishi 21 wanaodaiwa
kununuliwa vyeti, majina ya watu 10 waliopunguzwa kazini pamoja na
nyaraka zinazoonyesha stahiki zao.
Post a Comment