0

Mwanza. Tukiwa tunaelekea kuhitimisha mwaka 2017, mkoa wa Mwanza na viunga vyake vilitikiswa na matukio mbalimbali.

Miongoni mwa matukio yaliyobamba na kutikisa nyoyo za wakazi mkoani hapa ni vifo vya watu mbalimbali pamoja na mamilioni ya fedha ambayo idadi yake haikujulikana kuteketea ndani ya nyumba.

Juni 10 mwaka huu wakazi wa Mwanza waligubikwa na simanzi ya kifo cha milionea mmoja mkazi wa jiji la Mwanza, Maduhu Masunga (76) maarufu kwa jina la Mzee Shinyanga kuteketea kwa moto ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi pamoja na mamilioni yake.

Mzee huyo inadaiwa alifariki dunia wakati anajaribu kuokoa mamilioni hayo ya fedha aliyokuwa ameyaficha ndani ya nyumba hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi ilisema thamani ya mali na fedha zilizoteketea katika ajali hiyo haijafahamika na kwamba jeshi la polisi lilikuwa linaendelea na uchunguzi kubaini kiasi cha fedha hizo.

Pamoja na kiasi cha fedha kilichokutwa ndani hakijaweza kujulikana, Meneja wa Idara ya Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kanda ya Ziwa, James Machemba alisema kisheria fedha zote zinapaswa kuhifadhiwa kwenye taasisi za fedha ili zirejee kwenye mzunguko na hivyo kusisimua uchumi.

“Hata kama ni fedha zinazomilikiwa kihalali, ni kosa kisheria kuhifadhi kiasi kikubwa nyumbani; fedha zinatakiwa kuwa kwenye mzunguko na anayezihifadhi ndani anakwamisha maendeleo na uchumi wa Taifa,” alisema Machemba.

Akizungumza na gazeti hili akiwa nyumbani kwake mtaa wa Kirumba wilayani Ilemela, mke wa marehemu, Mariam Masanja (68) alisema pamoja na kuwa mzee huyo alikuwa akimiliki mali nyingi yakiwamo maghorofa na magari lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa anajua kiasi cha fedha alichokuwa nacho na mahala alipoweka fedha zake.

Mke wa marehemu pamoja na baadhi ya watoto waliozungumza na gazeti hili kila mmoja alidai kuwa hafahamu ni kiasi gani cha fedha alichokuwa anamiliki.

“Mzee Shinyanga alikuwa anatoa mahitaji yote muhimu kwenye familia, ikiwamo kusomesha watoto lakini hatukuwahi kujua kama fedha zote zinakaa ndani tena kwenye ndoo, hadi pale siku ya tukio zilipobainika zimeteketea kwa moto,” alisema Mariam.

Majambazi wauawa Mwanza

Tukio jingine lililoibua hisia kwa wakazi wa Mwanza ni baada ya jeshi la polisi mkoani Mwanza kufanikiwa kuwaua majambazi sita katika mtaa wa Fumagila, kata ya Igoma jijini Mwanza.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Julai 8 mwaka huu baada ya majambazi hao kurushiana risasi na askari waliokuwa doria, hivyo kufanikiwa kuyaua huku wawili wakifanikiwa kutoroka.

Kutokana na tukio hilo, wakazi wa mtaa huo waliingiwa na hofu hivyo kusababisha shughuli zao za kila siku kusuasua.

Mauaji ya wanandoa

Mauaji ya wanandoa nayo yalileta taswira mbaya kwa wakazi wa mkoani Mwanza baada watu wawili wakazi wa mtaa wa Kanyerere, kata ya Butimba kuuana kwa risasi.

Tukio hilo lilitokea Mei 25, mwaka huu baada ya Maximilian Tula (40) kumuua kwa kumpiga risasi mkewe Teddy Malulu kabla ya yeye kujimaliza.

Chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi kati yao.

Mbali na tukio hilo, matukio ya wanandoa kuuana yaliendelea baada ya wakazi wa kijiji cha Mwagiligili wilayani Sengerema, Kwilokeja Boniphace (35) kumuua mkewe Shija Luchagula (30) kwa kumpiga na kumnyonga kisha naye kujinyonga kwa kile kinachosemekana kuwa ni wivu wa mapenzi.

Matukio mengine yanayofanana na hayo zaidi ya saba yaliendelea kutokea katika maeneo mbalimbali mkoani humo.

Hiace yatumbukia ziwani

Oktoba 9 mwaka huu, wakazi wa mkoa wa Mwanza pia waliingiwa na simanzi kutokana na vifo vya watu 12 waliofariki dunia baada gari dogo la abiria maarufu kama daladala aina ya Toyota Hiace kutumbukia Ziwa Victoria katika Kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi.

Baadhi ya majeruhi walitoka salama na kulazwa katika Kituo cha Afya Bukumbi.

Majeruhi Yohana Ngabula alisema ajali hiyo ilisababishwa na dereva kuwa kwenye mwendo mkali.

“Tulimshauri dereva asiendeshe kwa kasi lakini hakutusikiliza hali iliyosababisha gari kufeli breki na kusababisha vifo hivyo,” alisema Ngabula.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Bukumbi, Dk Robert Shija alithibitisha kupokea miili ya watoto watatu na watu wazima tisa.

Miezi mitatu baadaye watu watano walifariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea jijini Mwanza ikihusisha gari aina ya Coaster na lori eneo la Buhongwa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 16, saa 3:30 usiku katika barabara ya Mwanza-Shinyanga kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana.

Wanawake wavishana pete

Tunaweza kusema kuwa ni tukio la funga mwaka baada ya jeshi la polisi mkoani hapa kuwatia nguvuni wanawake wawili waliodaiwa kuvishana pete za uchumba kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ambao ni, Milembe Suleiman (35) na Janeth Shonza (25) Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Gway Sumaye na kusomewa shtaka la kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja.

Wakili wa Serikali, Emmanuel Luvinga alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Agosti 31 wakiwa katika Hoteli ya Pentagon jijini Mwanza, kinyume cha kifungu cha 138 A cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 16 kama na marekebisho yake ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo namba 548/2017, Wakili Luvinga alidai kuwa washtakiwa hao waligusanisha ndimi zao ikiwa ni shara ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi kinyume cha sheria.

Aneth Mkuki (24) mkazi wa jijini Mwanza, naye alifikishwa mahakamani kwa shtaka hilo hilo na kifungu hicho hicho cha sheria baada ya kudaiwa kuwa mshereheshaji siku ya tukio hilo.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Richard Fabian (28) Mkazi wa Buzuruga Mwanza yeye ameshtakiwa kwa kosa la kusambaza picha ya video za tukio hilo la kuvishana pete, kinyume na Sheria ya Mtandao Kifungu cha 20 Kifungu Kidogo cha (1) (a) cha Sheria ya Mitandao namba 14 ya mwaka 2015.

Wakili Jebra Kambole anayewatetea washtakiwa hao aliiomba mahakama iwape dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yana dhamana.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Sumaye lakini akasema kwamba hawezi kutoa masharti ya dhamana kwa sababu shauri hilo lilipangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilbert Chuma ambaye hakuwapo.

Posted by Gambabway

Post a Comment

 
Top